Na mwandishi wetu
Wenyeji Zanzibar Heroes wameanza vyema michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kuichapa Kilimanjaro Stars bao 1-0 katika mechi iliyochezwa leo Ijumaa, Januari 3, kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.
Bao hilo pekee lilifungwa na kiungo wa Azam FC, Feisal Salum au Fei Toto dakika ya 52 akiitumia pasi ya Saleh Gumbo kabla ya kumtungua mlinda mlango wa Kili Stars, Metacha Mnata aliyeufuata mpira bila mafanikio.
Mpira uliozaa bao hilo ulitokana na makosa ya beki wa Kili Stars, Simfukwe Charles ambaye aliporwa mpira na Gumbo kabla ya kumpasia Fei ambaye aliujaza wavuni kwa mguu wa kushoto.
Awali timu zote zilionesha uhai na walikuwa ni Kili Stars walioanza kulisakama lango la Heroes mapema dakika ya 15 baada ya Idd Nado kufumua shuti ambalo kipa Yakoub Suleiman aliokoa kwa umahiri mkubwa.
Dakika tatu baada ya shambulizi hilo, Edson Katanga alimrudishia mpira kipa Mnata ambaye alichelewa na bado kidogo Fei Toto autumie mpira huo kuandika bao lakini hakuweza kuuwahi.
Heroes walifanya shambulizi lingine dakika ya 25 lililotokana na krosi ya Salum Khamis na Fei Toto kufumua shuti lililookolewa na Lameck Lawi wakati Mnata akiwa ametoka golini ingawa aliuwahi mpira huo akiwa mbali na goli lake.
Crispin Ngushi naye nusura aipatie Kili Stars bao katika dakika ya 45 baada ya kuuwahi mpira na kufumua shuti lakini kwa mara nyingine umahiri wa kipa Yakoub Suleiman ulikuwa kikwazo.
Dakika ya 49 Heroes walifanya shambulizi na Masoud Juma akiwa katika nafasi nzuri aliinasa pasi ya Hamad Hilika lakini shuti alilopiga lilitoka nje ya lango.
Michuano hiyo itaendelea kesho Jumamosi saa mbili usiku kwa mechi kati ya Kenya na Burkinafasso ambayo pia itapigwa kwenye Uwanja wa Gombani.
Soka Znz Heroes yailaza Kili Stars 1-0
Znz Heroes yailaza Kili Stars 1-0
Read also