Na mwandishi wetu
Bao pekee la mkwaju wa penalti iliyofungwa kiufundi na Jean Ahoua leo Jumanne kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam limezima ndoto za JKT Tanzania kugawana pointi moja moja na Simba katika Ligi Kuu NBC.
JKT ikilindwa vyema na kipa Yakoub Suleiman, aliyezuia mashuti ya mara kwa mara ya washambuliaji wa Simba, ilifanikiwa kumaliza dakika 90 za kawaida timu zikiwa hazijafungana.
Timu hiyo hata hivyo ilifanya kosa katika dakika sita za nyongeza, kosa ambalo lilizaa penalti iliyoipa Simba ushindi wa bao hilo pekee na pointi tatu muhimu za kujiimarisha kileleni mwa ligi hiyo ikifikisha pointi 37 katika mechi 14.
Kosa hilo lilitokana na mpira wa juu uliopigwa na Ahoua aliyempenyezea Shomari Kapombe ambaye wakati akikimbia kuelekea kwenye lango la JKT na kumuacha beki Mohammed Bakar, beki huyo alimshika Kapombe na kumuangusha chini akiwa eneo la penalti.
Kwa kosa hilo mwamuzi alimpa Bakar kadi ya njano kabla ya kujiridhisha katika rekodi zake na kumpa kadi nyekundu kwa sababu tayari alikua na kadi ya kwanza ya njano.
Ahoua alirudi nyuma akamzuga kipa kabla ya kufumua shuti lililojaa wavuni upande wa kushoto wa kipa huyo ambaye alijichanganya na kuonekana kama alishindwa kujua afanye nini ili kuokoa mpira huo.
Timu zote ziliuanza mchezo kwa kushambuliana kwenye kipindi cha kwanza ingawa Simba ndio waliofanikiwa kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa JKT na kama si umahiri wa kipa Suleiman, Simba wangetoka uwanjani na mabao mengi.
Katika dakika ya 16 Elly Mpanzu alipiga krosi safi lakini hakukuwa na mchezaji wa kumalizia na dakika moja baadaye, Ateba aliunganisha kwa kichwa krosi lakini Suleiman alikuwa imara na kuokoa.
JKT nao walifanya shambulizi dakika ya 22 baada ya nyota wa zamani wa Simba, Shiza Kichuya kumpasia Hassan Kapalata ambaye hata hivyo shuti lake lilitoka nje ya goli.
Kipindi cha pili Simba ilikianza kwa kuwatoa Awesu Awesu na nafasi yake kuingia Ahoua, baadaye wakatoka Mpanzu na Ateba na nafasi zao kuingia Mutale na Mukwala.
JKT nao wakafanya mabadiliko kwa kuwaingiza, Kichuya na Magulu na nafasi zao kuingia Matheo Anthony na Mohammed Bakar na baadaye akatoka Idd Gamba na kuingia nyota wa zamani wa Simba na Azam FC, John Bocco.
Simba nao waliendelea na mabadiliko kwa kumtoa Valentino Ouma na kumuingiza Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ na baadaye wakamalizia kwa kumuingiza Valentino Mashaka aliyechukua nafasi ya Deborah Fernandes.
Mabadiliko hayo yalionekana kuimarisha ulinzi kwa JKT wakati kwa Simba waliongeza mashambulizi na muda mwingi mpira ulikuwa langoni mwa JKT.
Mashambulizi hayo yalimuweka katika wakati mgumu kipa Suleiman wa JKT aliyekuwa na kazi ya kuokoa na kuchelewesha muda wakati Mussa Camara wa Simba alikuwa na kazi ndogo ya kuokoa mashambulizi machache na kupeleka mipira mbele kwa haraka huku akiwahimiza wachezaji waendeleze mashambulizi.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Singida Black Stars ikiwa nyumbani ilitoka na ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Ken Gold.
Ushindi huo umeifanya Singida Black kufikisha pointi 33 sawa na Yanga inayoshika nafasi ya pili na Azam FC inayoshika nafasi ya tatu wakati Singida ni ya nne kwa kuwa imezidiwa wastani wa mabao.
Kimataifa Ahoua azima ndoto za JKT
Ahoua azima ndoto za JKT
Read also