Manchester, England
Mshambuliaji wa Man City, Erling Haaland amejibebesha lawama kwa mwenendo mbaya wa timu hiyo hasa baada ya kipigo cha Jumamosi ingawa amemkingia kifua kocha Pep Guardiola.
Man City iliyoonekana kuwa dhaifu jana Jumamosi ililala kwa mabao 2-1 mbele ya Aston Villa hali inayozidi kuibua maswali kuhusu ongezeko la matokeo mabaya ya timu hiyo.
Mabingwa hao mara nne wa Ligi Kuu England au EPL hadi sasa wapo nafasi ya sita katika ligi hiyo na wapo nyuma ya Liverpool, vinara wa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi tisa.
Haaland ambaye hadi sasa ana mabao matatu tu msimu huu, akizungumzia mwenendo wa timu hiyo alisema anawajibika kufanya bidii na kuwa katika ubora ili kuisaidia timu.
“Kwanza najiangalia mimi mwenyewe, sijawa mwenye kufanya mambo mazuri kiasi cha kutosha, sikuwa mwenye kutumia nafasi zangu kufunga, lazima nifanye yaliyo bora, sijawa katika ubora unaotakiwa,” alisema Haaland.
Haaland alisema hawajawa wenye kujiamini japo wanafahamu umuhimu wa hilo na wanajua namna kutojiamini kunavyoathiri kila binadamu hivyo wanatakiwa wajiamini na kuwa na mtazamo chanya japo ni jambo gumu.
Matokeo mabaya ya Man City pia yanazidi kumuweka pagumu kocha Pep ambaye inaonekana kama ameishiwa mbinu za kuisaidia timu lakini Haaland anasisitiza kwamba timu ipo pamoja na kocha huyo.
“Atatafuta suluhisho, amekuwa akifanya jambo hilo kila mwaka, bado tuna imani naye, tunatakiwa kufanya bidii zaidi kwa wakati huu kuliko ilivyowahi kuwa,” alisema Haaland.
Pep amewapa wachezaji wake likizo ya siku mbili ili kuwaweka sawa kiakili na kukiri kwamba mwenendo mbaya wa timu hiyo ni jambo linalowasumbua wote vichwa vyao.