Na mwandishi wetu
Simba imeibugiza Kagera Sugara mabao 5-2 huku kumbukumbu ya kuvutia zaidi ikiwa bao la tatu la Fabrice Ngoma aliyeshangilia kwa kuwaonesha mashabiki ishara ya mabao matano.
Matokeo ya mechi hiyo ya Ligi Kuu NBC iliyochezwa leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, yanawafanya Simba, kushika usukani wa ligi hiyo wakiwa na pointi 34.
Simba waliandika bao la kwanza dakika ya 13 mfungaji akiwa beki wa kulia Shomari Kapombe aliyeinasa krosi ya beki mwenzake wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ na kuusukumiza mpira wavuni kwa guu la kulia.
Kagera wakipambana kutaka kusawazisha walijikuta wakipachikwa bao la pili dakika ya 44 mfungaji akiwa Jean Ahoua kwa mpira wa adhabu uliogonga mwamba wa juu kabla ya kuingia ndani.
Adhabu hiyo ilitolewa na mwamuzi baada ya Ahoua kuchezewa rafu na Abdallah Mfuko kwa kumzuia njiani wakati aAhoua kielekea kuonana na mlinda mlango wa Kagera Sugar, Ramadhan Chalamanda.
Ahoua ambaye ndiye nyota wa mchezo huo alionesha ufundi wa kuitumia mipira ya adhabu kwa kumchambua Chalamanda aliyeshtukia mpira umegonga mwamba na kuokolewa ukiwa tayari umevuka mstari wa goli.
Kagera walikianza kipindi cha pili kwa kuonesha shauku ya kurudisha mabao hayo ambapo dakika ya 48, Eric Mwijage aliambaa na mpira kwa kasi na kuwazidi mabeki wa Simba kabla ya kufumua shuti ambalo lilitoka nje ya lango.
Kasi ya Kagera iliendelea huku wakijiimarisha zaidi eneo la kati na kuidhibiti Simba na katika jitihada hizo dakika ya 52, Hijah Shamte alipewa kadi ya njano kwa kumchezea rafu nyota mpya wa Simba, Elly Mpanzu.
Mpanzu ambaye hiyo ni mechi ya kwanza akiwa na Simba, licha ya kuonesha uwezo wa kutengeneza mashambulizi na kuisumbua Kagera kwenye eneo la kati na mbele, alitolewa na nafasi yake kuingia Joshua Mutale.
Simba walifanikiwa kuigeuzia kibao Kagera kwa kuandika bao la tatu dakika ya 54 mfungaji akiwa Ngoma aliyeunganisha kwa kichwa kona iliyopigwa na Chasambi.
Ngoma ambaye naye pia alitolewa dakika chache baada ya bao hilo na kuingia Yusuf Kagoma, alishangilia kwa kucheza na kuwaonesha mashabiki ishara ya mabao matano ambayo ndiyo Simba waliyoyafunga.
Umahiri wa Chasambi kwa mara nyingine uliipatia Simba bao la nne katika dakika ya 66 alipomuunganishia pasi Jese Mukwala aliyeujaza mpira wavuni kwa shuti la mguu wa kushoto.
Baada ya kuingia bao hilo, kocha wa Simba Fadlu Davis alifanya mabadiliko akiwatoa Kapombe na kumuingiza Kelvin Kijili, Debora Fernandes na nafasi yake kuingia Muzamir Yassin.
Wakati Simba wakiwa katika kilele cha furaha, kocha wa Kagera, Mellis Medo wakati wote alionekana akiwahimiza wachezaji wake kutulia jambo ambalo walilifanya kwa kucheza pasi nyingi kama vile walikuwa wameshinda na hivyo wanachelewesha muda.
Mbinu hiyo ya Kagera ilizaa matunda dakika ya 79 walipopata bao la kwanza lililofungwa na Tareq Seif kwa shuti la chinichini baada ya kuinasa pasi ya Datus Peter.
Bao hilo liliwashtua Simba ambao walianza kuhaha kutafuta bao ambalo walilipata dakika ya 84 lililofungwa na Mukwala na kwa mara nyingine pasi ya Chasambi ikawa msaada.
Kagera nao waliendelea na utulivu na kuwashangaza mashabiki wa Simba kwa kuandika bao la pili lililofungwa na Cleophace Mukandala katika dakika ya pili ya nyongeza baada ya 90 za kawaida kumalizika.
Kimataifa Simba yaibugiza Kagera 5-2
Simba yaibugiza Kagera 5-2
Read also