Na mwandishi wetu
Simba imenyakua pointi tatu muhimu baada ya kuicharaza Ken Gold FC mabao 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa leo Jumatano kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Shujaa wa Simba katika mchezo huo alikuwa ni Leonel Ateba ambaye alifungua kitabu cha mabao ya timu yake katika dakika ya 34 kwa bao la mkwaju wa penalti.
Penalti hiyo ilitolewa baada ya kiungo wa Ken Gold, George Sangija kumchezea ndivyo sivyo kiungo wa Simba, Awesu Awesu katika eneo la hatari.
Dakika moja kabla ya timu hizo kwenda mapumziko Ateba aliandika bao la pili safari hii akiuunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Valentine Nouma.
Kipindi cha pili kila timu ilipambana kutengeneza nafasi lakini za kufunga lakini hakuna iliyoweza kubadili matokeo ya mchezo huo.
Kwa ushindi huo Simba ambao pia wanashiriki Kombe la Shirikisho Afrika wanakuwa wamefikisha pointi 31 katika mechi 12 za ligi hiyo.
Timu hiyo inashika nafasi ya pili ikiwa imetanguliwa na Azam FC wanaoshika usukani wakiwa na pointi 33 lakini wameizidi Simba kwa tofauti ya mechi mbili.
Kimataifa Simba yaicharaza Ken Gold 2-0
Simba yaicharaza Ken Gold 2-0
Read also