Nyon, Switzerland
Fainali za Kombe la Dunia za Wanaume za 2034 zitafanyika nchini Saudi Arabia wakati Hispania, Ureno na Morocco kwa pamoja wataandaa fainali hizo kwa mwaka 2030.
Sambamba na hilo, mechi tatu za fainali michuano hiyo kwa mwaka 2030, zitachezwa katika nchi za Argentina, Paraguay na Uruguay kwa ajili ya kumbukumbu ya miaka 100 ya Fifa.
Uamuzi huo uliotangazwa siku za nyuma ulithibitishwa rasmi leo Jumatano katika mkutano mkuu wa Fifa uliohusisha wajumbe wote wa mataifa 211 waliopiga kura kwa njia ya mtandao.
Nchi ya Norway ilitangaza kujitenga katika zoezi hilo kwa sababu ya kutokuwa na imani na taratibu za Fifa za kuteua nchi mwenyeji wa fainali hizo na si kwa sababu Saudi Arabia au Saudia imetangazwa kuwa mwenyeji.
Nayo Switzerland iliomba kupitia chama chake cha soka uwakilishi wao utambuliwe katika mukhtasari wa vikao vya mkutano mkuu.
Jana Jumanne Chama cha Soka Switzerland kilitoa taarifa kikidai kwamba kitaridhia Saudi Arabia kuwa mwenyeji wa fainali hizo lakini kikataka masuala ya haki za binadamu nchini humo yasimamiwe na Fifa pamoja na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Denmark nayo kupitia chama chake cha soka yaani DBU kilitangaza kuunga mkono taratibu zote za kuipa Saudi Arabia uenyeji wa fainali hizo lakini kikataka Fifa waangazie masuala ya haki za binadamu nchini humo.
Saudi Arabia imekuwa ikituhumiwa kwa kutumia fedha nyingi kwenye michezo kama kinga ya kuusafisha utawala wa kifalme na rekodi mbaya ya haki za binadamu.
Tayari Saudi Arabia imejenga viwanja vya soka vinne kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia 2034 na mpango uliopo ni kujenga viwanja 15.
Kimataifa Rasmi, Saudia mwenyeji Kombe la Dunia 2034
Rasmi, Saudia mwenyeji Kombe la Dunia 2034
Read also