Manchester, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola inaonekana amekata tamaa ya kubeba taji la Ligi Kuu England (EPL) msimu huu baada ya kudai kwamba huenda ni wakati wa timu nyingine kubeba taji hilo.
Man City baada ya kulala kwa mabao 2-1 mbele ya Brighton, kwa sasa imeachwa kwenye msimamo wa EPL kwa tofauti ya pointi tano na vinara wa ligi hiyo, Liverpool.
Kwa mara ya kwanza katika miaka yake 17 ya ukocha kwa timu za hadhi ya juu, Pep amepoteza mechi nne mfululizo na kwa Man City inapoteza mechi nne mfululizo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 18.
Muelekeo wa Man City msimu huu unaelekea kuvuruga rekodi nzuri ya timu hiyo kushinda mataji sita ya EPL kati ya saba yaliyopita hapo hapo wakiwa na rekodi ya kubeba mataji manne mfululizo.
Msimu huu hata hivyo unaonekana kuwa mgumu kwa timu hiyo ikiwa imepoteza mechi za ligi dhidi ya Bournemouth na Brighton na Tottenham kwenye Carabao na Sporting kwenye Ligi ya Mabingwa.
“Tunatakiwa kujaribu tena kushinda mechi zetu, kushindwa mechi nne mfululizo ni lazima tubadili mambo kwa haraka, ratiba imekuwa ngumu lakini ni suala la kushinda mechi,” alisema Pep.
Pep pia alisema kwamba huenda baada ya miaka saba ya kushinda mataji sita labda kuna timu ina haki ya kubeba taji hilo kwa mwaka mmoja.
Man City kwa upande mwingine inakabiliwa na tatizo kubwa la wachezaji majeruhi wakiwamo Ruben Dias, John Stones, Jeremy Doku na Jack Grealish pamoja na majeruhi wa siku nyingi Rodri na Oscar Bobb.
Majanga hayo ya wachezaji majeruhi yamemfanya Pep ampe nafasi kwa mara ya kwanza katika mechi ya EPL katika nafasi ya ulinzi, nyota wake wa miaka 19, Jahmal Simpson-Pusey.