Na Hassan Kingu
Yanga hadi sasa hawajaamini kama wamefungwa bao 1-0 na Azam FC, hawajaamini na hawataki kukubali kwamba mbali na Azam pia wamefungwa mabao 3-1 na Tabora United
Kilichowakuta wanaona kama si hadhi yao, wao si wa kufungwa na sasa wameanza kusaka mchawi kwa staili ya mihemko, wakati huo huo mahasimu wao Simba wakiendelea kuwananga kwa kila namna.
Mmoja wa wahanga ambaye amekuwa mjadala katika mihemko hiyo ni kocha Miguel Gamondi ambaye jina lake la Master Gamondi limeanza kuonekana si lolote mbele ya baadhi ya mashabiki wa Yanga.
Wapo mashabiki ambao wanaamini vipigo hivyo viwili vinatosha kuwa sababu ya timu hiyo kuachana na Gamondi na kusaka kocha mwingine.
Katika hilo tayari kocha kutoka nchini Algeria ameanza kutajwa na hata picha zake kutawanywa kwenye mitandao ya kijamii na vyanzo mbalimbali vya habari.
Ni baada ya vipigo hivyo ndipo tumeanza kusikia habari kwamba Gamondi haambiliki, ni baada ya vipigo hivyo tumeanza kusikia kuwa uwezo wa kocha huyo ni mdogo, vipigo pia vimemfanya aanze kulinganishwa na kutofautishwa na mtangulizi wake Nasreddine Nabi.
Gamondi ambaye jana aliimbwa na kupambwa kwa kila namna leo hali imekuwa tofauti, mechi mbili zimempa sura tofauti kabisa na sura aliyokuwa nayo jana.
Utajiri au uwezo wa kifedha wa Yanga nao unazidi kuzidisha mtazamo mbaya kuhusu Gamondi kwamba ana wachezaji wazuri na hivyo timu yake inapaswa kuishinda kila timu inayocheza nayo.
Hoja kuhusu matatizo yanayowakabili wachezaji wa kikosi cha kwanza wa timu hiyo ni kama vile zinaonekana si lolote si chochote badala yake tatizo ni uwezo wa kocha kuwatumia wachezaji waliopo kwa kuwa nao uwezo wao ni wa juu.
Kuumia kwa mabeki tegemeo wa timu hiyo, Shadrack Boka anayecheza upande wa kushoto na Yao Kouasi anayecheza upande wa kulia kumeiathiri Yanga lakini wako mashabiki ambao wanaamini hiyo haitoshi kuwa sababu ya timu yao kufungwa.
Kupewa kadi nyekundu na kukosekana kwa beki mwingine tegemeo wa kati, Ibra Bacca nako pia hakutoshi kuwafanya baadhi ya mashabiki kuamini kwamba hilo ni tatizo linaloifanya timu yao isipate matokeo mazuri.
Mashabiki hawa kwao tatizo la kupoteza mechi mbili ni la kiufundi na mhanga kwao ni Gamondi, anatakiwa aondoke na nafasi yake apewe kocha mwingine.
Ukiachana na Gamondi, mhanga mwingine ambaye ameanza kulalamikiwa ni wachezaji, hawa wanadaiwa kuanza kushuka viwango au kutocheza katika ubora wao.
Mhanga mmojawapo mkuu katika hilo ni Stephane Aziz Ki ambaye ukame wake wa mabao msimu huu umeanza kulalamikiwa hasa baada ya vipigo hivyo viwili.
Mengi ya Aziz Ki yameanza kuzungumzwa, wapo ambao wamekuwa akirusha mitandaoni picha za mchezaji huyo katika maisha yake binafsi akiwa maeneo ya starehe na kuzihusisha moja kwa moja na kushuka kwake kiwango.
Wengine wanakwenda mbali zaidi na kutaja jina la mtu ambaye wanaamini ndiye anayemkwaza mchezaji huyo asifunge au akose penalti au ubora wake ushuke (kama kweli umeshuka).
Kuna ambao ukiwasikiliza utadhani ni mashuhuda wa mchezaji huyo katika maisha yake ya kila siku ya nje ya uwanja, wanajua anaishi wapi na anafanya nini na anafanya na nani. Hoja za kiufundi zinazotolewa kwamba baadhi ya mabeki wameshamjulia Aziz Ki zinaonekana kutokubalika, badala yake mchezaji huyo anatakiwa afunge asipofanya hivyo sababu ya haraka inayotolewa ni kwamba ameshuka kiwango.
Ukweli ni kwamba taharuki iliyoibuka sasa ikipewa nafasi wakati huu ligi bado mbichi inaweza kuivuruga Yanga kuliko ilivyo sasa.
Hoja zote zinazotolewa na mashabiki kama hazitafanyiwa tathmini ya uhakika zinaweza kuwa mtaji mzuri wa mahasimu wa Yanga kuivuruga timu zaidi ya hiki kinachoonekana kwa sasa.
Upo uwezekano mkubwa kwamba hoja za kumsakama Gamondi na wachezaji wa Yanga zinatoka upande wa pili na kutumiwa ili kuitoa Yanga kwenye mstari na kibaya zaidi ni kwamba Yanga wenyewe wameingia katika mtego wa taarifa zisizo rasmi na kuziamini.
Taarifa hizo zisizo rasmi ni kama vile kikao kizito kimefanyika na maamuzi yamefanyika, Gamondi hana muda mrefu wa kuinoa Yanga.
Habari hizi za upande mmoja kutumia udhaifu wa upande wa pili kama jiwe ni utamaduni wa muda mrefu baina ya timu hizi.
Kilichopo ni kwamba Yanga hii ni timu nzuri, na japo vipigo vinashtua lakini uongozi usikubali taharuki na mihemko iliyoibuka iwe sababu ya kuivuruga timu yao.
Inaweza kuonekana jambo la kawaida na rahisi kumuondoa Gamondi na kuja na kocha mpya lakini huyo kocha mpya ajaye kazi yake inaweza kuwa ngumu na kumfanya ahitaji muda mrefu wa kupata timu ya ushindi.
Soka Vipigo vyazua mihemko Yanga
Vipigo vyazua mihemko Yanga
Read also