Madrid, Hispania
Kiungo wa Real Madrid, Jude Bellingham amelalamikia mabadiliko ya majukumu kuwa ndiyo yaliyomsababishia ukame wa mabao tangu kuanza kwa msimu huu.
Bellingham ambaye pia ni kiungo wa timu ya taifa ya England ametoa kauli hiyo baada ya kufunga bao lake la kwanza msimu huu Jumamosi hii timu yake ikiichapa Osasuna mabao 4-0 katika La Liga.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye dimba la Bernabeu, bao la Bellingham lilipatikana dakika ya 42 wakati mabao mengine matatu ya timu hiyo yakifungwa na Vinicius Jr.
Kabla ya bao hilo, Bellingham aliifungia Real Madrid mara ya mwisho mwishoni mwa msimu uliopita wa 2023-24, msimu ambao mchezaji huyo aliumaliza akiwa amefunga mabao 19.
“Najiona ni mwenye kufanya yale yale ninayoyafanya, lakini tofauti pekee ni kwamba nimefunga goli, watu wengi wamekuwa wakizungumzia hilo kwa sababu mwaka jana nilifunga magoli mengi lakini nafikiri sasa nacheza katika majukumu tofauti,” alisema Bellingham.
Bellingham alifafanua kuwa kwa sasa anafanya majukumu tofauti katika sehemu tofauti ya uwanja na kwamba atafanya lolote kwa ajili ya timu.
Mashabiki wa Real Madrid wameendelea kumuunga mkono mchezaji huyo licha ya ukame wa mabao na hata alipotolewa dakika ya 75 walisimama na kumpa heshima yake.
“Bado najiona kama mimi ni mtu wa kipekee katika dunia hii kwa kuichezea hii klabu, hata katika wakati mgumu bado nashukuru kwa kuwa hapa, kutoka nje na kupewa heshima, hilo najivunia,” alisema Bellingham.
Bellingham pia alimpongeza mchezaji mwenzake VinÃcius ambaye mabao yake matatu aliyofunga yamemfanya afikishe mabao manane hadi sasa baada ya kucheza mechi 12 za La Liga msimu huu.