Na mwandishi wetu
Simba imeanza kuonja ugumu wa Ligi Kuu NBC msimu huu wa 2024-25 baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Coastal Union katika mechi iliyopigwa Ijumaa hii kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge Dar es Salaam.
Hayo ni matokeo ya kwanza yasiyovutia kwa Simba tangu kuanza kwa msimu huu wa ligi baada ya kuwa tayari imeshinda mechi zake nne za awali na hivyo kujikuta ikikusanya pointi 13 badala ya 15 zilizotarajiwa na mashabiki wake.
Katika mechi hiyo, Simba ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ dakika ya 25 na Lionel Ateba kuongeza la pili kwa penalti dakika tano kabla ya timu kwenda mapumziko.
Matarajio ya Simba kutoka na pointi zote tatu yalianza kuvurugwa katika dakika ya 47 kwa bao lililofungwa na Abdallah Hassan wakati lile la kusawazisha lilifungwa na Ernest Malonga katika dakika ya 71.
Simba sasa itakuwa na kibarua kigumu cha kufunika kosa hilo hapo Oktoba 19 itakapoumana na hasimu wake wa soka nchini Yanga, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Ken Gold ikiwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, iliilaza JKT Tanzania kwa bao 1-0 wakati Mashujaa ikiwa nyumbani Lake Tanganyika ililala kwa bao 1-0 mbele ya Singida BS.
Soka Simba, Coastal zatoka sare ya 2-2
Simba, Coastal zatoka sare ya 2-2
Read also