Manchester, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amesema licha ya timu yake kuanza vibaya msimu huu kwa kupoteza mechi nne na kushinda mbili tu za Ligi Kuu England (EPL) bado hakuna sababu ya kupaniki.
Kocha huyo Mholanzi ametoa kauli hiyo baada ya timu yake kulala kwa mabao 3-0 mbele ya Tottenham Hotspur katika mechi ya mwisho ya EPL Jumapili iliyopita hali ambayo imeibua hofu.
Mwenendo mzima wa timu hiyo inayoshika nafasi ya 13 katika EPL unaonekana kukiweka pabaya kibarua cha kocha huyo ambaye takriban miezi minne iliyopita aliongezewa mkataba.
“Tutakuwa wenye mafanikio msimu huu, hakuna jambo rahisi lakini yanayotokea hayana sababu ya kunifanya nipaniki, tunaweza kulimaliza tatizo, hii timu inaweza kuyamaliza mambo haya,” alisema Ten Hag.
Ten Hag pia alisisitiza kwamba hana hofu ya usalama wa kibarua chake licha ya kupoteza mechi dhidi ya Spurs huku akikabiliwa na mechi ya Europa dhidi ya Porto pamoja na mechi ya EPL dhidi ya Aston Villa.
Kocha huyo badala yake alisisitiza kwamba hafikirii chochote na wala hana hofu, akifafanua kwamba walijenga mazingira ya umoja kati ya wamiliki na viongozi na wote wanayalinda mambo hayo.
“Tuna makubaliano ambayo wote tupo nyuma ya makubaliano hayo, tunajua kwamba mbinu yetu ni kuwaandaa wachezaji vijana ambao wapo katika kipindi cha mpito,” alisema Ten Hag.