Na mwandishi wetu
Yanga na Simba zimetoka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 kila moja katika mechi zao za Jumapili hii za Ligi Kuu NBC wakati Azam FC ikiambulia sare ya bila kufungana.
Simba iliyokuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma ilipata ushindi wa bao hilo pekee lililofungwa katika dakika ya 63 na Jean Ahoua kwa mkwaju wa penalti.
Penalti hiyo ilitolewa baada ya Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ kuchezewa rafu na kiungo wa Dodoma Jiji Salmin Hoza na mwamuzi Omar Mdoe kuamuru ipigwe penalti japo wachezaji wa Dodoma Jiji walipinga uamuzi huo.
Ushindi huo licha ya kuwa mwembamba lakini ni wa nne mfululizo kwa Simba na unaifanya timu hiyo ifikishe pointi 12 ikiwa haijapoteza hata mechi moja tangu kuanza kwa ligi hiyo msimu huu wa 2024-25.
Nao mahasimu wao Yanga kama ilivyo kwa Simba walineemeka na bao pekee la Maxi Nzengeli mbele ya KMC katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi tisa katika michezo mitatu na kama ilivyo kwa mahasimu wao Simba, Yanga nao hawajapoteza mchezo hata mmoja tangu kuanza kwa ligi.
Nao Azam walijikuta pagumu baada ya kubanwa na Mashujaa na kutoka sare ya bila kufungana katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Azam ambayo imetoka kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hiyo sasa inakuwa sare yake ya tatu tangu kuanza kwa ligi hiyo.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Singida Black Stars imeshindwa kutamba kwenye uwanja wake wa nyumbani wa CCM Liti baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na JKT Tanzania.
Soka Yanga, Simba ushindi mwembamba
Yanga, Simba ushindi mwembamba
Read also