Munich, Ujerumani
Klabu ya Bayern Munich imemfanyia vipimo mshambuliaji wake, Harry Kane aliyeumia enka jana Jumamosi katika mechi dhidi ya Bayer Leverkusen na kubaini kuwa tatizo si kubwa.
Kane, 31, ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya England alilazimika kutolewa dakika ya 86 katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye dimba la Alianz Arena na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Kuumia kwa Kane kulitokana na kugongana na Amine Adli wa Leverkusen na kuibua hofu kwamba Bayern ingemkosa nyota huyo ambaye hadi sasa ana mabao 10 katika mechi saba za mashindano yote msimu huu.
Timu ya madaktari wa Bayern hata hivyo baada ya kumfanyia vipimo leo Jumapili wamebaini kwamba tatizo si kubwa na mshambuliaji huyo anaendelea vizuri.
Habari zaidi zinadai kwamba Kane mwenyewe saa kadhaa baada ya mechi hiyo alinukuliwa akisema kwamba anatarajia kuwa fiti kwa ajili ya mechi ya Jumatano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo Bayern itakuwa mgeni wa Aston Villa.
Katika mechi dhidi ya Leverkusen, Bayern ilikuwa ya kwanza kutikiswa nyavu zake na Robert Andrich kabla ya kusawazisha kwa bao lililofungwa na Aleksandar Pavlovic.
Matokeo hayo hayajaitoa Bayern kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Ujerumani au Bundsliga ikifuatiwa na RB Leipzig kwa tofauti ya pointi mbili na mabingwa watetezi Leverkusen wanashika nafasi ya tatu wakiachwa nyuma na Bayern kwa tofauti ya pointi tatu.
Kimataifa Majeruhi Kane hali si tete
Majeruhi Kane hali si tete
Read also