Manchester, England
Kiungo wa Man City, Rodri atazikosa mechi zote za msimu huu kutokana na majeraha ya misuli ya mguu aliyoyapata Jumapili iliyopita.
Rodri, 28, aliumia Jumapili katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL) dhidi ya Arsenal iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2 baada ya kugongana na Thomas Partey.
Akithibitisha kuhusu mchezaji huyo, kocha wa Man City, Pep Guardiola alisema kwamba Rodri amefanyiwa upasuaji asubuhi ya leo Ijumaa na atakosa mechi zote za msimu huu.
“Amefanyiwa upasuaji asubuhi hii kwa hiyo atakuwa hapa msimu ujao, kwa msimu huu ndio amefika mwisho,” alisema Pep.
Pep aliwahi kusema kwamba mchezaji huyo hakuwa na mbadala katika kampeni zao za kulisaka taji la EPL msimu uliopita ambapo walifanikiwa kuwazidi waliokuwa wapinzani wao wakuu Arsenal na kubeba taji hilo mara ya nne mfululizo.
Katika msimu huo, Rodri alikosa mechi tano za timu hiyo na kati ya hizo Man City ilipoteza nne na kwa mantiki hiyo huenda pengo hilo likawaathiri kwa mara nyingine msimu huu.
“Ni bahati mbaya tumepata habari zisizofurahisha lakini haya mambo huwa yanajitokeza, tutakuwa naye kumuunga mkono hatua kwa hatua wakati akipata matibabu ili apone, alichotupa hatuna mchezaji anayefanana naye,” alisema Pep.
Pep alisema kwa sasa klabu inalifanyia tathmini tatizo la mchezaji huyo kabla ya kuamua kama watasajili mchezaji mwingine katika dirisha dogo la Januari na kutafuta namna ya kucheza mechi nyingi zilizobaki bila ya kuwa na mchezaji wao muhimu.