Na mwandishi wetu
Simba imeanza kwa sare ya 0-0 na Ahly Tripoli katika mechi yake ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyopigwa leo Jumapili mjini Tripoli, Libya.
Wachezaji wa Ahly walikuwa wakishangiliwa kwa nguvu na mashabiki wao walioujaza uwanja, waliuanza mchezo kwa kutawala vyema dakika 20 za kipindi cha kwanza kwa pasi nyingi dhidi ya Simba.
Pasi za Ahly katika kipindi hicho zilizalisha mashambulizi kadhaa ambayo yalianzia pembeni hasa kupitia kwa Mohamed Abdusalam na mshambuliaji wa kati, Christopher Mabululu ambaye alilichachafya mara kadhaa lango la Simba.
Katika kipindi hicho mabeki wa Simba wakiongozwa na mlinda mlango Mussa Camara na beki wa kati Che Malone Fondoh walifanikiwa kuyadhibiti mashambulizi hayo kabla ya Simba kuanza kujibu mapigo.
Mashambulizi ya Simba yaliitikisa Ahly hasa kuanzia dakika ya 30 baada ya Jean Ahoua kuunasa mpira akiwa karibu na eneo la kati na kumchungulia kipa wa Ahly aliyetoka kidogo katika eneo lake kabla ya kufumua shuti la juu ambalo bado kidogo liipatie Simba bao.
Kipindi cha pili, Simba ilijiimarisha kwa kocha Fadlu Davids kufanya mabadiliko akianza kuwatoa Ateba na baadaye Joshua Mutale na nafasi zao kuingia Valentino Mashaka na Kibu Dennis ambao walizidi kuipa uhai Simba katika eneo la ushambuliaji na baadaye kumtoa Edwin Balua na nafasi yake kuingi Augustine Okehefa.
Ahly nao hawakuwa nyuma katika kusaka bao ambapo Fondoh alilazimika kufanya juhudi binafsi kuutoa mpira mbele ya mshambuliaji wa Ahly ambaye alikuwa akielekea kukutana na kipa wa Simba kabla ya kuanguka chini na kuanza kulalamika akitaka timu yake ipewe penalti.
Tukio hilo lilizua tafrani ya muda mfupi kwa wachezaji wa Ahly kumzonga mwamuzi ambaye hata hivyo alishikilia msimamo wake wa kuipa timu hiyo kona akikataa kwamba Fondoh alicheza rafu ndani ya eneo la penalti.
Simba waliendelea kufanya mabadiliko kwa kuwatoa Ahoua na Deborah Fernandes na nafasi zao kuingia Chamou Karaboué na Donald Ngoma wakati Ahly nao wakati huo huo walimuingiza mshambuliaji wao tishio Ahmed Akrawa ambaye alikuwa akiimbwa na mashabiki wa timu hiyo.
Mshambuliaji huyo aliongeza uhai kwenye safu ya ushambuliaji na dakika chache kabla ya kutimua dakika 90, nusura aipatie timu hiyo bao baada ya kuunganisha krosi iliyotokea upande wa kulia wa Ahly lakini mpira alioupiga kwa kichwa uligonga mwamba na kurudi uwanjani.
Matokeo ya mechi hiyo yanaweza kuwa msaada kwa Simba kusonga mbele kama wataweza kuutumia vyema uwanja wa nyumbani katika mechi ya marudiano itakayopigwa wikiendi ijayo.
Kimataifa Simba, Ahly Tripoli zatoka sare
Simba, Ahly Tripoli zatoka sare
Read also