Na mwandishi wetu
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo Jumanne imetoka kifua mbele baada ya kuichapa Guinea mabao 2-1 katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025.
Katika mechi hiyo iliyopigwa mjini Yamoussoukro, Ivory Coast, Guinea wanaochezea nchini humo mechi zao za kimataifa, ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 56 lililofungwa na Mohammed Bayo.
Bayo kabla ya kufunga bao hilo alizuiwa vyema na Ibrahim Bacca ambaye katika harakati za kuzuia alianguka chini na Bayo kumpiga chenga kabla ya kufumua shuti lililomshinda mlinda mlango wa Stars, Ally Salim.
Guinea wakiwa katika hali ya furaha walinyamazishwa na Fei Toto katika dakika ya 61 baada ya nyota huyo wa Azam FC kuonesha kwa mara nyingine umahiri wake wa kufumua mashuti ya mbali alipofumua shuti lililomshinda kipa wa Guinea, Ibrahim Cone.
Bao hilo halikuwasumbua Guinea ambao waliendelea kucheza soka lao la kujiamini na kuutawala mchezo kwa pasi nyingi huku wakilisogelea lango la Stars na wachezaji wa Stars wakiwa na kazi ya kutibua mashambulizi.
Guinea hata hivyo walijikuta katika wakati mgumu kwenye dakika ya 89 baada ya Stars kufanya shambulizi ambalo lilizaa shuti lililopigwa na Fei Toto na kuokolewa na kipa wa Guinea na mpira kumkuta Mudathir Yahya aliyeujaza wavuni.
Mudathir kama kawaida yake baada ya kufunga bao hilo alikimbia na kuchukua kilinda ugoko au ‘shin guard’ na kushangilia kama mtu anayezungumza na simu.
Katika mechi ya leo kocha wa Stars Hemed Suleiman ‘Morocco’ alifanya mabadiliko kadhaa akiwatoa Dickson Job aliyeumia na nafasi yake kuingia Bakari Mwamnyeto ambaye aliziba vyema pengo la Job katika eneo la ulinzi.
Baadaye Morocco aliwatoa Edwin Balua na Waziri Junior na Clement Mzize na nafasi zao kuingia Paschal Msindo, Himid Mao na Cyprian Kachwele, mabadiliko ambayo yalizidi kuipa uhai Stars na kuwa timu yenye kutengeneza mashambulizi yaliyowaweka pagumu Guinea.
Kwa ushindi huo Stars ambayo katika mechi yake ya kwanza dhidi yaEthiopia ilitoka sare ya 0-0, sasa imefikisha pointi nne na kushika nafasi ya pili nyuma ya DR Congo yenye pointi sita.
Kimataifa Stars yainyuka Guinea 2-1
Stars yainyuka Guinea 2-1
Read also