Dortmund, Ujerumani
Baada ya Uholanzi kutolewa na England katika nusu fainali Euro 2024 kwa mabao 2-1, kocha wa timu hiyo, Ronaldo Koeman amelalamikia matumizi ya VAR akidai teknolojia hiyo inaua soka.
Koeman alichukizwa na bao la England lililotokana na penalti iliyopigwa na Harry Kane baada ya mchezaji huyo kuchezewa rafu na mwamuzi kutumia VAR kujiridhisha kuhusu rafu hiyo na hatimaye England kupewa penalti.
Katika mechi hiyo, Uholanzi waliandika bao la kwanza kupitia Xavi Simons kabla ya England kupata penalti dakika ya 18 baada ya Denzel Dumfries kumkaba ndivyo sivyo Kane ambaye pamoja na hilo alifanikiwa kupiga mpira ambao ulipaa.
England iliendelea kupambana na kupata bao la pili na la ushindi lililofungwa katika dakika ya 90 na Ollie Witson ambaye aliingia akitokea benchi.
Awali mwamuzi wa mechi hiyo, Felix Zwayer hakutoa penalti lakini baadaye alitoa penalti hiyo aliposhauriwa kuangalia picha za VAR na ndipo alipotoa ishara ya penalti ambayo hatimaye iliipa England bao la kusawazisha.
“Kwa mtazamo wangu ile haikutakiwa kuwa penalti, aliupiga mpira, nafikiri sasa hatutoweza kucheza soka kwa katika namna nzuri na hii ni kwa sababu ya VAR, hakika inaharibu soka,” alisema Koeman.
Naye beki wa Uholanzi, Virgil van Dijk alisema kwamba penalti waliyopewa England ilibadili kila kitu katika mchezo huo.
“Nafikiri penalti ilikuwa tukui kubwa, England walipata hali ya kujiamini kupitia penalti, nafikiri maamuzi mengi hayakuwa mazuri kwetu, lakini sitaki kumzungumzia mwamuzi,” alisema Van Dijk ambaye pia ni beki wa Liverpool.
Kwa upande wake beki wa zamani wa Man United na England ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka, Gary Neville alisema kwamba Uholanzi wana kila sababu ya kuona wameumizwa.
“Nikiwa kama beki nafikiri ni uamuzi usiofdaa, hakuna namna unaweza kusema ile ilikuwa penalti, alikwenda kuzuia mpira, kwangu mimi ile si penalti,” alisema Neville.
Akizungumzia tukio hilo hilo, mshambuliaji wa zamani wa Newcastle na England ambaye kwa sasa pia ni mchambuzi, Alan Shearer alisema ni wazi kulikuwa na kugusana lakini beki wa Uholanzi alikuwa akijaribu kuzuia mpira.