Na mwandishi wetu
Stephanie Aziz Ki hatimaye amemaliza utata baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea Yanga na hivyo kumaliza mijadala na vijembe miongoni mwa mashabiki wa soka nchini.
Mashabiki wa Yanga na Simba katika siku za karibuni wamekuwa wakilumbana na kucharurana kuhusu hatma ya mchezaji huyo kama angeendelea kuichezea Yanga au angeachana na timu hiyo.
Mjadala huo ulizidi kuwa mkubwa baada ya mwenyekiti wa Yanga, Hersi Said kuweka wazi siku chache zilizopita kuwa mchezaji huyo hakuwa amesaini mkataba mpya baada ya ule wa awali kufikia ukomo.
Ukimya wa Aziz Ki na kauli ya Hersi kwa pamoja vilizidisha mijadala mitandaoni na vijiweni huku mashabiki wa Yanga wakionekana kushambuliwa kwa kupigwa vijembe lakini kwa sasa yote hayo yamekwisha.
Aziz Ki ambaye amemaliza msimu uliopita w 2023-24 akiwa mfungaji bora, zilikuwapo habari kwamba alikuwa akitakiwa na klabu kadhaa za Afrika hapo hapo ikadaiwa Simba nao walikuwa wakifuatilia kwa karibu maendeleo yake ili wamchukue kama angaitema Yanga.
Yote hayo yamekwisha na kwa sasa mashabiki wa Yanga wanajiona washindi wakitembea vifua mbele baada ya kushinda vita ya mitandaoni na vijiweni kuhusu hatma ya Aziz Ki.
Vyanzo vya habari vya klabu ya Yanga Jumatano hii vilitawaliwa na habari ya kiungo huyo mshambuliaji kwa kuuhakikishia umma kwamba msimu ujao huduma ya mchezaji huyo itaendelea kuonekana mitaa ya Jangwani na Twiga jijini Dar es Salaam yalipo makao makuu ya klabu ya Yanga.
“Nimeamua kuendelea kubaki Yanga ili kukamilisha majukumu katika klabu hii,” ilisomeka taarifa ya mchezaji huyo huku akisisitiza shauku yake ya kuuanza msimu ujao wa 2024-25.
Soka Aziz Ki amaliza utata
Aziz Ki amaliza utata
Read also