Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imeahidi kuisuka timu tishio kuelekea msimu ujao kwa ajili ya kuvuka malengo na kile walichokifanya kwenye msimu wa 2023-24 uliomalizika hivi karibuni.
Meneja habari na mawasiliano Yanga, Ali Kamwe amezungumza hayo na GreenSports Ijumaa hii kuhusiana na hilo alipokuwa akifafanua kuhusu uzinduzi wa kitabu maalumu cha historia ya Yanga utakaofanyika Jumamosi hii.
“Kwanza niwaambie wanachama, wapenzi na mashabiki wa Yanga kwamba uongozi wao upo makini na unafanya tathmini zake kwa weledi mkubwa, sisi hatuendeshwi na propaganda za mitandao na maneno ya wachambuzi kwa ajili ya kutuingiza ‘chaka’ katika usajili.
“Safari hii uongozi wetu umejikita kuifanyia kazi ripoti ya benchi la ufundi kuhakikisha tunakiongezea thamani na ubora kikosi tulichonacho. Tuliyasema haya baada ya msimu uliopita kumalizika na kilichotokea msimu huu kimeonekana kwa hiyo tunajiandaa zaidi kuelekea msimu ujao na mashabiki wasiwe na wasiwasi kabisa,” alisema Kamwe.
Pia, Kamwe alieleza kitabu watakachozindua kitakuwa kimesheheni maswali na historia kamilifu ya Yanga kikiwa kimesheheni matukio ya kutosha na hakiajaacha kitu.
“Hii klabu ina miaka 89 toka kuanzishwa kwake, katika miaka 89 yametokea matukio mengi sana, kwa hiyo ni safari ya milima na mabonde, furaha na simanzi, na ukiangalia miaka 89 hiki kimekuwa kilio kikuu wa cha Wanayanga kupata historia ya klabu yao.
“Kwa hiyo kazi hii tumeianza miezi saba iliyopita kuhakikisha tunakusanya historia ya Yanga, hakijaachwa kitu, hii klabu imesimuliwa kwa vitu vingi ikiwemo harakati za ukombozi wa taifa hili na haya yote watayafaidi na kunufaika nayo Wanayanga kupitia kitabu hiki,” alisema Kamwe.
Kitabu hicho kinazinduliwa wakati ambao Yanga imetoka kuweka historia ya kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza msimu wa 2022-23.
Yanga pia imefika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu pamoja na kutwaa ubingwa wa 30 wa Ligi Kuu msimu huu ikiwa ni timu ya kwanza Tanzania kufikisha idadi hiyo.