Na mwandishi wetu
Mbunge wa Jimbo la Mlalo, Rashid Shangazi ameeleza kuwa amejiuzulu nafasi yake ya mjumbe wa bodi ya wakurugenzi Simba SC kwa maslahi mapana ya klabu hiyo.
Shangazi ameeleza hayo leo Ijumaa jijini Dar es Salaam akiuthibitishia umma juu ya fununu hizo zilizoanza kushika hatamu tangu juzi akisema ameyafanya hayo kama sehemu ya uwajibikaji kutokana na kuyumba kimatokeo kwa timu hiyo takriban misimu miwili mululizo sasa.
“Nimejiuzulu kwenye Bodi ya Klabu ya Simba na nataka niuthibitishie umma wa Simba na wanamichezo kwamba ni kweli nimemwandikia barua mwekezaji wetu, Mohammed Dewji ya kumuomba nijiondoe katika bodi tangu Juni 2, nimefanya hivyo kama sehemu ya uwajibikaji kwa namna ambavyo hatukuwa na matokeo mazuri takriban katika misimu hii miwili.
“Sasa kama kiongozi nimejitathmini nimeona inawezekana kuna mahali ambapo hatukufanya vizuri sana basi uungwana ni kupisha ili mwenyekiti na mwekezaji wetu aweze kutengeneza safu upya ya bodi ambayo itaisimamia Simba iweze kurudisha utimamu wake wa kuchukua vikombe,” alisema Shangazi.
Shangazi ambaye aliteuliwa kwenye nafasi hiyo Julai, 2021 imeelezwa kuwa si peke yake ambaye amechukua maamuzi hayo kwani safu nzima ya wajumbe walioteuliwa na Dewji imejiuzulu.
Mbali na shangazi wengine wanaotajwa kuchukua uamuzi huo ni Dk Raphael Chegeni, Hamza Johari, Zulfikar Chandoo na mwenyekiti Salum Abdallah ‘Try Again’ ambaye nafasi yake inatajwa kuchukuliwa na mtendaji mkuu wa zamani Simba, Barbara Gonzalez.
Taarifa zaidi zinafafanua kuwa ndani ya saa 24 mpaka 48, safu mpya ya wajumbe upande wa mwekezaji itatangazwa huku wajumbe waliopitishwa na wanachama kwenye mkutano mkuu wakiendelea na majukumu yao kama kawaida.