Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa PSG na timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe amesema kitendo cha yeye kujiunga na Real Madrid ni kutimia kwa ndoto yake ya muda mrefu.
Mbappe, 25, anajiunga na timu hiyo kwa mkataba wa miaka mitano, mpango ambao utakamilishwa rasmi mara baada ya mkataba wa mchezaji huyo na PSG kufikia ukomo Juni 30 mwaka huu.
Imeelezwa kuwa katika mkataba wake na Real Madrid, Mbappe atakuwa akilipwa Pauni 13 milioni kwa msimu pamoja na marupurupu mengineyo ikiwamo pesa ambazo zitatokana na matangazo yatakayohusu picha zake.
“Hakuna anayeweza kujua jinsi nilivyofurahishwa, ndoto yangu imekuwa kweli, nina furaha na najivunia kujiunga na klabu ya ndoto zangu,” alisema Mbappe.
Mbappe anajiunga na Real Madrid na kuikuta ikiwa na taji la 15 la Ligi ya Mabingwa Ulaya ambalo ililibeba Jumamosi iliyopita baada ya kuilaza Borussia Dortmund mabao 2-0 katika mechi ya fainali.
Hatua ya Mbappe kujiunga na Real Madrid inatajwa kuwa mwanzo mwingine wa zama mpya za kinachoitwa Galacticos katika klabu hiyo kwa kufanya usajili wa wachezaji wa hadhi ya juu duniani.
Katika hilo, Mbappe ataungana na washambuliaji wa Brazil, Vinicius Jr, Rodrygo na Endrick ambaye kama alivyo Mbappe naye ni usajili mpya, kundi hilo hilo pia yumo kiungo wa England, Jude Bellingham.