Na mwandishi wetu
Kocha wa Ihefu FC, Mecky Maxime amesema hana cha kuwalaumu wachezaji wake kwa kupoteza mechi yao ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho CRDB dhidi ya Yanga.
Maxime alisema kwamba wachezaji hao walifanya kila alichowaagiza na kufanya mchezo huo kuwa mgumu akiamini hata mashabiki pia wamevutiwa na hilo.
Ihefu ilipoteza mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha kwa kufungwa bao 1-0 dakika ya 100 baada ya mechi hiyo iliyoisha kwa suluhu katika dakika 90 za awali kuongezwa dakika 30 za ziada.
“Nisemme tu ulikuwa mchezo mzuri, ukiwalaumu wachezaji utakuwa huwatendei haki, ni mchezo wa mpira tumepata nafasi sisi tena nzuri kuliko wao tumeshindwa kuzitumia, wao wamepata wametumia.
“Sina cha kuwadai wachezaji wangu, wamenipa kila nilichokuwa nakitaka lakini basi ni matokeo ya mchezo tu wenyewe, lakini nafikiri hata watazamaji wamefurahia mechi,” alisema Maxime.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ambaye kikosi chake kitavaana na Azam FC kwenye mchezo wa fainali ya michuano hiyo amesema amefurahishwa na uvumilivu wa wachezaji wake kwa kupambana na timu nzuri kama Ihefu ingawa amekiri kutofurahishwa na uwanja waliochezea.
“Ulikuwa mchezo mgumu kwenye kipindi cha kwanza ambapo tulitengeneza nafasi kama nne na wao walifanya hivyo, kipindi cha pili nafikiri tulicheza sana mpira lakini walizuia vizuri na kutufanya tushindwe kufunga.
“Nikawaambia wachezaji wangu watulie wasipate preshA sababu kuna dakika 30 nyingine na nafikri Ihefu walishaanza kuchoka ikawa rahisi kidogo kwetu lakini kiukweli uwanja si rafiki kwa mchezo kama huu au wa fainali maana hata Ihefu sidhani kama walifurahia,” alisema Gamondi.
Soka Maxime awatetea wachezaji Ihefu
Maxime awatetea wachezaji Ihefu
Read also