Manchester, England
Ligi Kuu England (EPL) msimu wa 2023-34 umefikia tamati leo Jumapili kwa Man City kubeba taji ililokuwa ikilipigania na Arsenal baada ya kuibwaga West Ham mabao 3-1.
Arsenal kabla ya mechi ya leo ilikuwa imezidiwa na Man City kwa pointi mbili na ilitakiwa ishinde mechi yake na Everton huku ikiombea Man City ipoteze lakini mambo yakawa tofauti licha ya Arsenal kuichapa Everton mabao 2-1.
Ushindi huo unaifanya Man City kuweka rekodi ya kulibeba taji hilo kwa mara ya nne mfululizo ingawa ndoto zao za kubeba mataji matatu kama msimu uliopita hazijafanikiwa baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Man City bado ina nafasi ya kubeba taji la pili iwapo itaishinda Man United katika fainali ya Kombe la FA ambayo imepangwa kuchezwa Mei 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Wembley.
Ushindi wa Man City umetokana na mabao ya mchezaji bora wa msimu huu EPL, Phil Foden ambaye alifunga mabao mawili katika dakika ya pili na ya 18 wakati bao pekee la West Ham lilifungwa na Kudus dakika ya 42.
Mara baada ya filimbi ya kumaliza mchezo kupulizwa, mashabiki wa Man City waliokuwa nyumbani Ettihad walilipuka kwa shangwe wakijivunia mafanikio ya timu yao baada ya upinzani mkali walioupata kutoka kwa Arsenal.
Kwa kubeba taji la EPL kwa mara ya nne, Man City wanakuwa wameweka rekodi ya kipekee ambayo haijawahi kuwekwa na timu yoyote ya England tangu kuanza kwa ligi ya hadhi ya juu ya soka kwa England zaidi ya miaka 100 iliyopita.
Wakati Man City ikibebeba taji, timu za Luton Town, Burnley na Sheffield United tayari zimeshashuka daraja na msimu ujao zitashiriki ligi ya Championship.
Matokeo ya mechi za mwisho EPL leo Jumapili ni kama ifuatavyo…
Arsenal 2-1 Everton
Brentford 2-4 Newcastle
Brighton 0-2 Man United
Burnley 1-2 Nottingham Forest
Chelsea 2-1 Bournemouth
Crystal Palace 5-0 Aston Villa
Liverpool 2-0
Luton Town 2-4 Fulham
Man City 3-1 West Ham
Sheffield United 0-3 Tottenham
Kimataifa Man City yabeba taji EPL
Man City yabeba taji EPL
Read also