Na mwandishi wetu
Kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ameendelea kusisitiza kuwa hajali kupitwa idadi ya mabao na kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki katika mbio za kuwania kiatu cha ufungaji bora kwa kuwa anaangalia zaidi mafanikio ya kikosi chake.
Fei amezungumza hayo leo Ijumaa baada ya kupitwa na Aziz Ki kwa idadi ya mabao akiwa amefunga mara 14 na kumuacha Fei akiwa na mabao 13.
Fei hajafunga bao hata moja katika mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu NBC tangu alipofunga mara ya mwisho dhidi ya Yanga waliposhinda kwa mabao 2-1 wiki kadhaa zilizopita.
“Mimi katika ufungaji nafunga ili kusaidia timu yangu, kwa hiyo ninapopata nafasi ya kufunga nafanya hivyo si kwa kushindana na mtu kwamba yeye kanizidi nianze kumuangalia sana, mimi naangalia timu yangu kuipambania ili kupata matokeo zaidi,” alisema Fei mchezaji wa zamani wa Yanga.
Fei pia aligusia ushindani wao wa ubingwa dhidi ya Yanga akifafanua kuwa licha ya wao kuwa wa pili kwa pointi 51 baada ya mechi 23 dhidi ya vinara Yanga wenye pointi 55 kwa mechi 21 lakini mechi saba zilizosalia kabla ya pazia la ligi kufungwa, zinaweza kutoa tafsiri halisi ya nani bingwa.
“Kwa sare yetu ya 0-0 na Mashujaa bado haiwezi kueleza kwamba tumemaliza mbio za ubingwa, bado kuna michezo ipo mbele, bado zimebakia mechi saba sasa hivi kwa hiyo tutaendelea kupambana katika michezo ya mbele iliyosalia ili tufike kwenye nafasi nzuri sababu mbio za ubingwa bado ziko wazi,” alisema Fei.