Munich, Ujerumani
Mshambuliaji wa Bayern, Munich, Harry Kane amesema kwamba msimu huu unaweza kuwa ni msimu waliofeli kama hawatabeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Bayern leo Jumatano itakuwa nyumbani ikiiumana na Arsenal katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwa ni mechi ya marudiano baada ya sare ya 2-2 katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye dimba la Emirates.
Taji pekee kubwa lililobaki kwa Bayern ili kulinda heshima yao ni la Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuwa tayari wamepoteza taji la Ligi Kuu Ujerumani yaani Bundesliga ambalo tayari limebebwa na Bayer Leverkusen.
“Bado tuna nafasi ya kubadili mambo katika msimu huu na kuufanya msimu uwe mkubwa na hiyo ni kama tutashinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya,” alisema Kane.
“Ukweli ni kwamba kwa msimamo wa klabu utakuwa ni msimu tuliofeli kama hatutoweza kubeba taji lolote mwaka huu kwa sababu matarajio ni kushinda taji lakini tunachoweza kufanya ni kwenda na hali hiyo hadi mwakani na kujaribu kubadili mambo,” alisema Kane.
Kane mshambuliaji wa zamani wa Tottenham hakuwahi kushinda taji lolote kubwa tangu aanze kucheza soka la hadhi ya juu na ilitarajiwa angefanya hivyo msimu huu na Bayern lakini timu hiyo imekwama licha ya kuwa na rekodi ya kubeba taji la Bundesliga mara 11 mfululizo.