Na mwandishi wetu
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema hana presha kuelekea mechi hiyo na Simba maarufu Kariakoo au Dar Derby kwa kuwa anakwenda kutengeneza timu bora kuhakikisha inaibuka na ushindi katika mchezo huo.
Gamondi amezungumza hayo Jumatatu hii mara baada ya kurejea Dar es Salaam wakitokea Mwanza walikopata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Singida Fountain Gate, mechi iliyopigwa Jumapili iliyopita.
Gamondi alisema anafahamu wana mechi ngumu mbele yao lakini ana matumaini ya kufanya vizuri kutokana na maandalizi na mwendo wa timu yake huku pia akiwa hajihusishi na mitandao ya kijamii kwa kuwa inachangia kukuza presha ya mechi hiyo.
“Mimi nafanya kazi katika weledi, sisikilizi watu wanasemaje, nahitaji kuandaa timu vizuri kwa namna inavyowezekana katika njia sahihi ili tushinde mechi japo naiheshimu Simba na naheshimu kila timu inayoshiriki ligi.
“Kiukweli sina presha yoyote na sifuatilii mitandao ya kijamii ndiyo maana unaona sina presha sababu nafikiri moja ya kitu kibaya cha mitandao ni kuleta presha, kila mtu anataka kuongea analotaka na kwenye mpira si wengi wanaouelewa lakini kila mmoja atataka kuweka maoni yake na wakati mwingine ndivyo soka lilivyo kila mmoja anataka kukosoa,” alisema Gamondi.
Wakati Gamondi akizungumza hayo, Simba yenyewe imerejea pia Dar ikitokea Singida ilikotoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Ihefu.
Meneja Habari wa Wekundu hao, Ahmed Ally amesema wanafahamu mechi hiyo ni ngumu na inatokana na matokeo ya ushindi ya Yanga kwa sasa lakini pia ukubwa wa mchezo wenyewe ila watajipanga kuhakikisha wanapambana na kupata matokeo.