Madrid, Hispania
Mshambuliaji wa Real MadrId, Vinicius Junior amejikuta akitokwa machozi mbele ya waandishi wa habari baada ya kukiri kwamba kadhia ya ubaguzi wa rangi dhidi yake inampunguzia shauku ya kucheza soka.
Vinicius Jr, ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Brazil, hata hivyo alisema pamoja na kadhia hiyo kuelekezwa zaidi kwake na mashabiki lakini hana nia ya kuacha kucheza soka katika Ligi Kuu Hispania maarufu La Liga.
Mchezaji ambaye mkataba wake na Real Madrid unaisha mwaka 2027, amejikuta mara kadhaa akizomewa na mashabiki wa timu pinzani tangu kuanza kucheza soka Hispania akiwa na klabu hiyo kwa takriban miaka mitano sasa.
“Nimekuwa hapa muda mrefu nikishuhudia jambo hili, najisikia mwenye huzuni zaidi, najikuta nikipungukiwa zaidi na zaidi shauku ya kucheza, kila malalamiko yanapofikishwa naona hali ni mbaya lakini nalazimika kuja hapa na kuiweka hadharani sura yangu,” alisema Vinicius Jr.
Mchezaji huyo alisema kwamba aliomba msaada Uefa, Fifa, Conmebol, CBF, wote wanaweza kupambana na ubaguzi wa rangi lakini tatizo analoliona Hispania ni kwamba ubaguzi wa rangi si jinai.
Vinícius alikuwa akizungumza jana Jumatatu mjini Madrid kabla ya mechi ya Brazil na Hispania ambayo imeandaliwa na mashirikisho ya soka ya nchi hizo kwa lengo la kuamsha ari ya kupambana na kadhia ya ubaguzi wa rangi.
“Nina hakika Hispania si nchi ya kibaguzi lakini wapo wabaguzi, wengi wao wapo kwenye viwanja vya soka, ni lazima tubadilike kwa sababu wengi wao hawajui ubaguzi ni nini, nina miaka 23 na nalazimika kuwafundisha watu wengi wa Hispania kuhusu ubaguzi,” alisema Vinicius Jr.
Vinicius Jr alisema kucheza soka ni muhimu lakini kupiga vita ubaguzi wa rangi pia ni muhimu na kutaka watu wa jamii tofauti waishi maisha ya kawaida vinginevyo anaweza kuishia katika klabu yake na kucheza soka tu lakini kitu pekee anachotaka ni kuona kila mtu anaisha maisha yake ya kawaida bila kudhihakiwa.