Paris, Ufaransa
Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps (pichani) ameelezea kufurahishwa kwake na kitendo cha kocha wa PSG, Luis Enrique kumuweka benchi mshambuliaji tegemeo wa timu hiyo, Kylian Mbappe.
Mbappe ambaye pia ni mshambuliaji tegemeo wa timu ya taifa ya Ufaransa amekuwa akiwekwa benchi katika mechi za hivi karibuni za PSG kwa kile ambacho, Enrique anaamini kuwa timu yake inatakiwa ianze kuishi bila ya mshambuliaji huyo.
Katika mechi tatu za hivi karibuni za Ligi 1, Mbappe amekuwa akitupwa benchi na kupewa muda mchache wa kucheza, mechi hizo zote ziliisha kwa sare lakini Enrique ameshikilia msimamo huo bila kujali matokeo hayo.
Akizungumzia hali hiyo, Deschamps amesema kwamba kwa kuzingatia idadi ya mechi ambazo mchezaji huyo amecheza kuna suala zima la kuwa fiti katika mashindano makubwa jambo ambalo ni muhimu.
Deschamps anaamini kuwekwa benchi kwa Mbappe kutamsaidia kuwa fiti zaidi wakati wa fainali za Kombe la Ulaya 2024 au Euro 2024 zitakazoanza kutimua vumbi Juni mwaka huu nchini Ujerumani.
“Ni vizuri akiwa anapata nafasi ya kucheza lakini kucheza kila baada ya siku tatu kuna ile hali ya mchoko ingawa sina hofu na kasi ya Mbappe na hayo ni maamuzi ya kocha wake,” alisema Deschamps.
Tangu Mbappe atangaze kutoongeza mkataba na PSG baada ya msimu huu huku akitajwa kuelekea Real Madrid, Enrique amewahi kusema kwamba kuna siku timu hiyo itamkosa Mbappe hivyo ni muhimu kujiandaa na maisha bila ya mchezaji huyo.