Na mwandishi wetu
Rais wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa msaada wake katika klabu hiyo inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Taarifa ya Mo iliyopatikana leo Jumatano Aprili 23, 2025 ilielezea shukrani za klabu hiyo kwa mchango wa usafiri na malazi kuelekea mchezo wao wa marudiano dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini.
Simba itarudiana na timu hiyo Jumapili ijayo katika mechi ya pili ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho ikiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 ilioupata Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Katika taarifa hiyo, Mo ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa klabu hiyo, alisema Simba inatambua na kuthamini juhudi za Rais Samia katika sekta ya michezo nchini hasa mchezo wa soka.
Mo alitolea mfano wa goli la mama ambalo huhusisha zawadi ya Sh milioni 10 kwa kila goli linalofungwa kwenye mechi za kimataifa akisema jambo hilo limekuwa chanzo cha hamasa na ari kwa wachezaji na mashabiki.
Sambamba na Rais Samia, Mo pia alitoa shukrani zake kwa Wizara ya Fedha pamoja na Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa namna wizara hizo zilivyoratibu safari ya Simba.
Mo pia alitoa shukran kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Reli Tanzania (TRL).
Iwapo Simba itafanikiwa kuitoa Stellenbosch itaumana katika fainali na mshindi wa mechi kati ya RS Berkane na CS Constantine.
Kimataifa Mo amshukuru Rais Samia
Mo amshukuru Rais Samia
Read also