Madrid, Hispania
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amezungumzia mambo yake ya baadaye katika klabu hiyo akisisitiza lolote linawezekana wakati huu timu yake ikichuana na Barcelona kuwania mataji ya La Liga na Kombe la Mafalme.
Ancelotti amekuwa katika kipindi kigumu tangu timu yake itolewe na Arsenal kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kipigo cha jumla cha mabao 5-1.
Real Madrid imeachwa na Barcelona kwa tofauti ya pointi nne katika La Liga zikiwa zimebaki mechi sita kabla ya kufikia tamati ya kwa ligi hiyo, pia Jumamosi itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya timu hiyo kwenye Kombe la Mfalme.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari leo Jumanne, Aprili 22, 2025 kabla ya kuumana na Getafe kwenye La Liga, Ancelotti alisema timu yake inaweza kubeba mataji yote hayo mawili.
Kuhusu presha ya nafasi yake ya ukocha, Ancelotti ambaye mkataba wake na Real Madtid unaishia 2026 alisema hali hiyo na yote yanayoendelea ni kama kichocheo kwake.
Kocha huyo badala yake aliwapa mashabiki wa timu hiyo habari njema kuhusu mshambuliaji Kylian Mbappe aliyeumia enka akisema anaendelea vizuri na anaweza kucheza mechi ya fainali ya Kombe la Mfalme.
“Katika soka lolote linawezekana, je mnashangazwa na mambo yote yanayotokea, hakuna kinachonishangaza mimi, kama ninavyosema wakati wote, naipenda hii kazi, nilipenda nilivyokuwa hapa awamu ya kwanza (2013 hadi 2015) napenda hii awamu ya pili kuanzia 2021 na nataka awamu hii iendelee kadri inavyowezekana,” alisema Ancelotti.
Ancelotti pia alisema kwamba ikifika siku ambayo kazi yake itafikia mwisho atakuwa mwenye kushukuru na kuvua kofia yake katika klabu hiyo kwani hiyo ndiyo hali halisi.
Kocha huyo Mtaliano amejijengea heshima kwa kuiwezesha Real Madrid kubeba mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini msimu huu umekuwa mgumu huku habari ya kutimuliwa kwake ikipamba moto siku hadi siku.