Madrid, Hispania
Baada ya kuitoa Real Madrid katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kutua nusu fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-1, kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amemkumbuka mwalimu wake Pep Guardiola.
Arsenal jana Jumatano ilifuzu hatua ya nusu fainali kwa kuichapa Real Madrid mabao 2-1 katika mechi ya pili ya robo fainali baada ya kushinda kwa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza.
Real Madrid ikiwa nyumbani Santiago Bernabeu ikilala kwa mabao ya Bukayo Saka ambaye pia alikosa penalti na Gabriel Martinelli aliyefunga la pili wakati bao pekee la Real Madrid likifungwa na Vinicius Junior.
Akimzungumzia Guardiola, Arteta alisema alimpigia simu mapema kocha huyo ambaye alidai anaendelea kufurahia ukaribu wao kikazi baada ya kufanya naye kazi Man City kwa miaka mitatu.
“Nilimpigia simu mapema (jana Jumatano) kwa sababu niko hapa na yeye namshukuru, nikiwa mchezaji na baadaye kocha amekuwa akinipa hamasa, nimekuwa na miaka minne mizuri pamoja naye na nitaendelea kumshukuru wakati wote,” alisema Arteta.
Kwa ushindi huo, Arsenal sasa inasubiri kuumana na PSG ya Ufaransa katika mechi ya kwanza ya nusu fainali itakayopigwa Aprili 29.
Akizungumzia mambo yajayo ya timu yake katika hatua waliyofikia, Arteta alisema kwa sasa wataendeleza wimbi la ushindi kwa sababu ari yao ipo vile vile.
“Kwa sasa tunatakiwa kuendelea kufanya tulichokifanya (ushindi) kwa sababu nadhani bado tuna ari ile ile,” alisema Arteta.
Arteta alisema jukumu lao ni kuwafanya watu wao wawe na furaha na anaamini watu hao wanajivunia wachezaji na timu na kilichobaki sasa ni wao kuangalia mambo ya mbele zaidi ya walipofikia sasa.
Naye Saka aliyepiga penalti kwa staili ya panenka na kukosa, alisema jambo hilo hutokea na kwamba alijaribu kufanya kitu tofauti lakini ikashindikana baada ya kipa Thibaut Courtois kuwa makini.
Kwa Arsenal hii inakuwa mara ya kwanza kufikia nusu fainali ya ligi ya mabingwa tangu mwaka 2009 wakati kwa Real Madrid wanakosa hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2020.