Mexico City, Mexico
Beki wa zamani wa Real Madrid, Marcelo amesema timu hiyo si ya kufutwa moja kwa moja wakati huu ikiwa na kibarua kigumu cha kupindua meza katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Real Madrid ina kazi ngumu ya kuupanda mlima baada ya kulala kwa mabao 3-0 mbele ya Arsenal Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa Enmirates katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Marceloa ambaye ana rekodi ya kubeba mataji matano ya ligi ya mabingwa akiwa na Real Madrid anaamini hakuna jukumu ambalo ni kubwa zaidi kwa klabu hiyo.
“Huwezi kuifuta moja kwa moja Real Madrid, ingawa mabao matatu ni mengi lakini wakati wote huwa naifikiria Real Madrid na nina imani kubwa kwa timu hiyo kwamba inaweza kujibu mapigo, Real Madrid ni Real Madrid na inaweza kushinda,” alisema Marcelo.
Marcelo ambaye kwa sasa yuko nchini Mexico akijiandaa kucheza mechi ya El Clasico ambayo itahusisha wachezaji wa zamani wa Real Madrid na Barcelona, alisema katika mechi ya marudiano, Real Madrid itakuwa na faida ya kuwa nyumbani kwenye dimba la Bernabeu.
“Mechi ya marudiano itakuwa Bernabéu, mashabiki wataiunga mkono kwa nguvu na wachezaji wanaamini inawezekana, ingawa ni kweli hatujui nini kitatokea bali tuna imani na Real Madrid kujibu mapigo,” alisema Marcelo.
Marcelo aliongeza kwa kusema kuwa anadhani ushindi upo katika damu za wachezaji wa Real Madrid na ni kama vile ni jambo ambalo wanafundishwa mara tu wanapoanza kuvaa jezi ya timu hiyo.
“Nafikiri mara tu tunapojiunga na Real Madrid tunafundishwa kutokata tamaa na hilo kwa wakati wote linakuwa kwenye damu zetu, ni kufanya juhudi, kuvumilia, kujitoa kila siku pamoja na kuungwa mkono na mashabiki, ni kati ya vitu vinavyosaidia mambo yaende,” alisema Marcelo.