Na mwandishi wetu
Kipa Musa Camara ameibuka shujaa kwa kuokoa mikwaju miwili ya penalti na kuiwezesha Simba kufuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuitoa Al Masry ya Misri kwa penalti 4-1.
Ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam Jumatano hii Aprili 9, 2025, Simba ilitoka na ushindi wa mabao 2-0 katika dakika 90 za kawaida hivyo kuingia kwenye mikwaju ya penalti baada ya timu hizo kuwa na matokeo ya jumla ya sare ya mabao 2-2.
Sare hiyo ya jumla imekuja baada ya Simba kulala kwa 2-0 katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo iliyopigwa, Ismailia, Misri, Jumatano iliyopita.
Mikwaju ya penalti
Simba ndio waliokuwa wa kwanza kupiga penalti iliyopigwa na Jean Ahoua ambaye alikwenda taratibu na kuujaza mpira wavuni kwa shuti la mguu wa kulia lililomshinda kipa, Mahmoud Gad.
Baada ya hapo Camara akaonesha ushujaa wake kwa kuokoa kwa miguu shuti la chinichini lililopigwa na Mido Gaber wakati Simba wakafunga penalti ya pili iliyopigwa kiufundi na Steven Mukwala.
Mukwala alirudi nyuma na kumchambua vyema kipa ambaye alijikuta akiruka upande wake wa kulia na mpira kujaa wavuni upande wa kushoto.
Al Masry walifanikiwa kupata bao katika penalti yao ya pili mfungaji akiwa Ben Youssef wakati Simba nao wakapata bao kwenye penalti ya tatu mfungaji akiwa Kibu Denis.

Camara kwa mara nyingine akaonesha umahiri wake kwa kuokoa penalti ya tatu ya Masry iliyopigwa na Mahmoud Hamada na kipa huyo kuruka upande wa kulia na kuuwahi mpira.
Baada ya hapo Shomari Kapombe akakamilisha hesabu kwa kuifungia Simba penalti ya nne ambayo ilifanya uwanja ulipuke kwa shangwe kutoka kwa mashabiki wa Simba na kuipa Simba ushindi wa 4-1 moja kwa moja hadi nusu fainali.
Kapombe baada ya kufunga penalti hiyo alikimbiliwa na wachezaji wenzake na benchi zima la ufundi na kushangilia na mchezaji huyo ambaye alivua jezi na kubaki na fulana ya ndani iliyoandikwa Jesus 100% yaani Yesu asilimia 100.
Dakika 90 zilivyokuwa
Katika dakika 90 za kawaida, Simba waliandika bao lao la kwanza dakika ya 22 mfungaji akiwa Elly Mpanzu wakati bao la pili lilifungwa na Steven Mukwala dakika ya 32.
Simba kama ilivyokuwa katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo, kwa mara nyingine ilifanikiwa kuutawala mchezo na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini tatizo lilikuwa katika umaliziaji.
Kwa jinsi hali ya mchezo ilivyokuwa Simba walikuwa na kila sababu ya kumaliza dakika 90 wakiwa washindi kwa zaidi ya mabao matatu na kusingekuwa na sababu ya kuingia kwenye penalti.

Al Masry kama kawaida yao walionekana kuzidiwa na kutumia mara kwa mara mbinu ya kuchelewesha muda kwa kujiangusha na wakati mwingine kuingia katika mzozo na watu wa huduma ya kwanza.
Kutokana na matukio hayo kujitokeza mara kwa mara, haikushangaza mechi kuchezwa kwa dakika 10 za nyongeza baada ya 90 za kawaida kukamilika.
Rais Samia awapongeza
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kupitia mtandao wa X (Twitter) aliipongeza Simba kwa ushindi huo ambao aliutaja kuwa ni burudani kwa Watanzania wote.
“Pongezi za dhati kwa Klabu ya Simba kwa ushindi katika mchezo wa mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ushindi wenu ni furaha kwa mashabiki wenu na burudani kwa Watanzania wote. Ninawatakia kila la kheri katika nusu fainali,” ilijieleza taarifa hiyo ya rais.
Baada ya ushindi huo, Simba sasa inasubiri kucheza mechi ya nusu fainali na mshindi wa mechi kati ya Zamalek ya Misri na Stellenbosch ya Afrika Kusini.