Manchester, England
Kipa wa Man United, André Onana amesema hatoruhusu maamuzi yake uwanjani yatokane na presha za mashabiki baada ya kushutumiwa kwa kukaa na mpira muda mrefu.
Onana amejikuta akitupiwa lawama na baadhi ya mashabiki wa Man United ambao wanaamini kipa huyo ana tabia ya kukaa na mpira muda mrefu wakati timu yake inapokuwa na nafasi ya kufanya shambulizi.
Kuna wakati kipa huyo amejikuta akipigiwa kelele na mashabiki na wengine kuguna na moja ya matukio ya kukumbukwa ni kwenye mechi ya Jumapili dhidi ya Man City iliyoisha kwa sare ya 0-0.
Akijibu malalamiko hayo ya mashabiki, Onana ambaye pia ni kipa wa timu ya taifa ya Cameroon alisema hawezi kuharakisha kufanya maamuzi kama hajafikiri maamuzi hayo kuwa ni sahihi au la.
Onana alisema kinachofanywa na mashabiki hakiwezi kuathiri maamuzi yake awapo uwanjani kwa sababu maamuzi ambayo anafanya ni kwa ajili ya kuisaidia timu.
“Kuna wakati nafanya maamuzi sahihi na kuna wakati nafanya makosa, ninapoona wachezaji wangu wanahitaji kupumzika lazima nijipe muda, ninapoona kuna uhitaji wa kuharakisha mchezo nafanya haraka,” alisema Onana.
Aliongeza kwamba kuna wakati hasa kipindi cha pili timu pinzani wakiwa wanamiliki mpira kwa kiasi kikubwa kuliko wao hapo analazimika kuwapa nafasi wachezaji wake wapumue.
Baada ya kutoka sare na mahasimu wao wa Manchester, Man United wtaaeleke Ufaransa ambapo keshokutwa Alhamisi wataikabili Lyon katika robo fainali ya Europa Ligi.