Na mwandishi wetu
Bao pekee la Pacome Zouzoua limetosha kuizamisha Coastal Union na kuipa Yanga ushindi wa 1-0 na kuifanya iendelee kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC.
Katika mechi hiyo iliyopigwa leo Jumatatu Aprili 7, 2025 kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge, Dar es Salaam, Pacome alifunga bao hilo katika dakika ya 35 akiitumia krosi ya Maxi Nzengeli.
Bao hilo limetosha kuifanya Yanga kunyakua pointi zote tatu na kufikisha jumla ya pointi 64 wakati Pacome akiendelea kung’ara kwa mabao katika ligi hiyo.
Sambamba na bao hilo, Pacome ambaye sasa anakuwa amefikisha mabao manane katika ligi hiyo, pia ndiye aliyeibuka mchezaji bora wa mechi ya leo.
Ushindi huo pia umeifanya Yanga kuiacha Simba inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi saba ingawa hadi sasa timu hiyo imecheza mechi 24 za ligi hiyo wakati Simba imecheza mechi 22.
Baada ya mechi hiyo kocha wa Yanga, Miloud Hamdi aliisifia timu yake kwa kupata ushindi ingawa alikiri kuwa wanahitaji kuiimarisha safu yao ya ushambuliaji kwa namna ambavyo wameshindwa kuzitumia nafasi walizotengeneza.
Kwa upande wa kocha msaidizi wa Coastal Union, Joseph Lazaro yeye aliwapongeza wachezaji wake kwa namna walivyocheza kwa kuwapa wakati mgumu Yanga.
Kimataifa Pacome aizamisha Coastal Union
Pacome aizamisha Coastal Union
Read also