Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Simba imezungumza na mhubiri maarufu Tanzania, Boniface Mwamposa ili awe mgeni maalum wa mechi yao ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry ya Misri.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi Aprili 5, 2025 na msemaji wa klabu hiyo, Ahmed Ally akiwa jijini Dar es Salaam kwa ziara inayoaminika kuwa na lengo la kuitangaza mechi hiyo.
Mwamposa au Bulldozer ambaye pia waumini wake wanamwita kwa jina la mtume ni miongoni mwa wahubiri wenye ushawishi mkubwa miongoni mwa waumini wa dini ya kikristo nchini.
Akizungumzia uamuzi wa kumualika Bulldozer na kauli yake kuonekana kwenye vyanzo vya habari vya klabu ya Simba, Ally alisema safari hii wamedhamiria kualika kila mtu mwenye mchango kwenye jamii.
“Safari hii tumedhamiria Ubaya Ubwela na tunaalika kila mtu mwenye mchango kwenye jamii hii, wachawi wengi ndugu zangu, kuna watu wamekunja nafsi, kwa hiyo namtangaza mgeni mwingine maalum, Mtume Boniface Mwamposa. Tunafanya naye mazungumzo.” alisema Ally.
Katika kuwataka mashabiki wa Simba kuhudhuria kwa wingi katika mechi hiyo, Ally pia alinukuliwa akisema kwamba ni lazima wanasimba wajitofautishe na mashabiki wa timu nyingine kwa kutobaki nyumbani siku ya mechi.
“Siku hiyo unabaki nyumbani unafanya nini, tujitofautishe an mashabiki wa timu nyingine, tofauti ya wao na sisi siku hiyo wao wanabaki nyumbani na sisi tunakwenda Uwanja wa Mkapa,” alisema Ally.
Mgeni mwingine maalum katika mechi hiyo ni rais wa TFF, Wallace Karia ambaye pia ni rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) na mjumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Simba itaumana na Al Masry katika mechi ya pili ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, mechi itakayopigwa Aprili 9, 2025 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo iliyopigwa Aprili 2, 2025, Ismailia, Misri, Simba ikiwa ugenini ililala kwa mabao 2-0.