Munich, Ujerumani
Kiungo mshambuliaji wa Bayern Munich, Thomas Muller (pichani) hatimaye ameamua atahitimisha rasmi safari yake ya miaka 25 katika klabu hiyo mara baada ya kumalizika kwa msimu huu.
Muller, 35, ataachana na klabu hiyo akiwa na rekodi ya kihistoria akishika namba moja kwa kuichezea mechi nyingi, 743, lakini pia anashika nafasi ya tatu kwa kuifungia mabao mengi, 247.
Kiungo huyo mshambuliaji ambaye wakati mwingine anacheza nafasi ya mshambuliaji wa pili, aliibukia katika akademi ya Bayern hadi kupanda katika kikosi cha timu kubwa mwaka 2008.
Muller ambaye mkataba wake unafikia ukomo mwishoni mwa msimu huu, ana rekodi ya kubeba mataji 33 na Bayern yakiwamo mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na 12 ya Ligi Kuu Ujerumani maarufu Bundesliga.
“Imekuwa ni safari ya kipekee, iliyoambatana na uzoefu wa aina yake, changamoto kubwa na mafanikio yasiyosahaulika,” alisema Muller.
Akizungumzia anachotaka cha kumuaga baada ya msimu huu, Muller alisema hilo liko wazi kwani angependa awe na mataji ambayo watayafurahia pamoja likiwamo taji la ligi ambalo kwa pamoja watalirudisha mjini Munich.
Kwa upande wa timu ya taifa ya Ujerumani, Muller ameichezea timu hiyo mara 131 na kuifungia mabao 45 na mwaka 2010 kwenye fainali za Kombe la Dunia alishinda kiatu cha dhahabu.
Muller pia alikuwamo katika kikosi cha Ujerumani kilichoshiriki fainali za Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil na kubeba taji hilo.