London, England
Mshambuliaji wa zamani wa Man United na timu ya taifa ya England, Wayne Rooney amesema kuwa ilikuwa bado kidogo ajiunge na Barcelona mwaka 2010.
Katika kipindi hicho Barelona au Barca ilisifika duniani kote kwa soka la uhakika huku ikibeba mataji ikiwa na mshambuliaji nyota Lionel Messi na viungo Xavi na Iniesta.
Akizungumza katika kipindi cha michezo cha BBC, Rooney pia alisema kwamba Real Madrid na Chelsea nazo zilimtaka lakini ilikuwa Barca chini ya Pep Guardiola ndiyo iliyomvutia zaidi.
“Nilipowaambia Man United mwaka 2010 kwamba sitaki kusaini mkataba mpya na kuwasilisha ombi la uhamisho, klabu tatu zilikuja zikitaka kunisajili,” alisema Roney.
“Manchester City imekuwa ikizungumzwa mara kwa mara kuwa ni mojawapo lakini sikuwahi kudhani kwamba ilikuwa chaguo langu, timu zilizowasilisha maombi ya kunitaka ni Real Madrid, Chelsea na Barcelona,” alisema Rooney.
Rooney alisema kwamba katika fikra zake alikuwa tayari kuondoka Man United na kwenda kucheza soka Hispania na mazungumzo ya awali yalishaanza kufanyika.
Pia Rooney alisema mpango wa kujiunga na Real Madrid nao kwa siku kadhaa ilionekana wenye kufanikiwa lakini alikuwa akiifikiria zaidi Barcelona na namna ambavyo angefiti katika kikosi kilichokuwa na Messi, Iniesta, Xavi na Sergio Busquets.
Rooney ambaye kabla ya kusajiliwa Man United alikuwa akiichezea Everton tangu utotoni, alisema kwamba mwishowe aliamua kubaki Man United lakini alivutiwa zaidi na Barca iliyokuwa na kikosi bora wakati huo na kila mchezaji angependa kucheza katika timu hiyo.