Athens, Ugiriki
Mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) na rais wa kwanza wa IOC anayetokea Afrika, Kirsty Coventry (pichani juu) ameahidi kuwalinda wanamichezo wanawake.
Katika miaka 130 ya historia ya IOC, ndoto ya kumpata rais mwanamke huenda haikuwahi kufikiriwa ukiachilia mbali mwanamke huyo awe ni mwenye kutoka katika bara la Afrika.
Mambo hata hivyo yamekuwa tofauti kupitia uchaguzi wa IOC uliofanyika Machi mwaka huu nchini Ugiriki kwa Kirsty ambaye pia amekuwa waziri nchini Zimbabwe kuibuka kidedea.
Kwa wananchi wa Zimbabwe ushindi wa Kirsty, unawakumbusha hali ilivyokuwa miaka 20 ilyopita wakati Kirsty ambaye kwa sasa ana miaka 41, aliposhinda medali ya dhahabu katika mchezo wa kuogelea.
Katika Michezo ya Olimpiki nchini Ugiriki miaka 20 iliyopita jina la Kirsty lilitamba na kuibua shangwe Zimbabwe na Afrika alipotwaa medali ya dhahabu katika mchezo wa kuogelea.
Machi 20 mwaka huu, Kirsty amewapa tena furaha wananchi wa Zimbabwe na Afrika kwa baada ya kushinda kiti cha urais wa IOC na sasa anasubiri Juni mwaka huu ili kuanza rasmi majukumu mapya ya ubosi wa IOC akichukua nafasi ya Thomas Bach (pichani chini) .
Ushindi wake ulimkumbusha mwaka 1992 akiwa msichana mdogo wa miaka tisa akiangalia Michezo ya Olimpiki ya Barcelona kwenye televisheni, hakuwahi kuwaza kama ingefika wakati akawa rais wa IOC.

Ushindi wake haujaibua furaha pekee bali pia kuna hali ya mshangao kwa kuwa hakuna au ni wachache mno waliokuwa na matarajio kama angeweza kuibuka kinara na kumrithi Bach.
Akizungumzia mikakati yake ndani ya IOC baada ya ushindi, Kirsty alisema atawalinda wanamichezo wanawake pamoja na kila kipengele cha michezo ya wanawake.
Katika hilo pia amefafanua kwamba hakuna jipya kwani amekuwa akikabiliana na wanaume wabishi tangu akiwa na umri wa miaka 20.
Zaidi ya hilo, Kirsty ameahidi kufanya kazi na mashirikisho ya kimataifa akitaka IOC kujipa jukumu la kiuongozi zaidi kwa kuunda vikosi kazi ambavyo vitafanyia tathmini kila kazi wanayoifanya.
Kirsty pia alikumbushia medali yake ya mwaka 2004 na ushindi wa urais wa IOC kwa kusema kwamba Ugiriki ni nchi yenye bahati kwake.
“Niliheshimiwa kwa mafanikio ya mwaka 2004 hapa Athens, inaonekana Ugiriki ni nchi ya bahati kwangu,” alisema Kirsty.
Kirsty pia alisema kwamba yeye si mwanamke wa kwanza kujitokeza katika kuwania nafasi hiyo na mmoja wao ambaye amesaidia kumpa hamasa ya kuitaka nafasi hiyo ni Anita DeFrantz ambaye alikuwapo wakati wa uchaguzi huo.
Alisema anajivunia kumfanya Anita awe na jambo la kujivunia kwa kuwa amemhamasisha na kumuongoza tangu wakati anaingia katika harakati za Olimpiki mwaka 2013.
“Najua itanichukua muda kidogo kuwa sawa hapa lakini mwanamke kama yeye huwa anafungua njia kwa wanawake wengine kama mimi na nataka nami nifungue njia kwa wanawake wengine vijana hasa kwa kuwa mimi ni mama wa watoto wawili wa kike,” alisema Kirsty.
Kuhusu mume wake
Akimzungumzia mume wake, Kirsty alimsifu kwamba ana mume wa kipekee na kuongeza kwamba kwa pamoja wana jukumu la kufanya maamuzi na wamekuwa ni watu wa kushirikiana.
“Mimi na mume wangu lazima tuwe wenye kufanya maamuzi, hata nilipopewa kazi ya Waziri wa Vijana, Michezo na Sanaa wa Zimbabwe, tulifahamu kwamba tunajitoa kufanya kazi ya kila siku,” alisema Kirsty.
Akizungumzia ushindi wa Kirsty, mtangulizi wake, Bach alisema IOC imempata mtu sahihi katika sehemu sahihi akiamini kuwa ushindi wa kiongozi huyo ni ishara ya mshikamano katika harakati za Olimpiki.