Na mwandishi wetu
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Walace Karia amewapongeza viongozi wapya wa Chama cha Soka Iringa (IRFA) walioachaguliwa hivi karibuni katika mkutano mkuu wa uchaguzi.
Katika taarifa iliyosainiwa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo imewataja viongozi hao kuwa ni Cyprian Kuyava aliyechaguliwa kuwa mwenyekiti na Joel Musiba (makamu mwenyekiti).
Wengine ni Abousufian Sillia (mjumbe wa mkutano mkuu), Davis Wapalila, Rehema Mhehe na Victoria Mwenda ambao wamechaguliwa katika nafasi za ujumbe wa kamati ya utendaji.
Karia amewataka viongozi hao kusimamia maendeleo ya soka mkoani Iringa akiwataka kuwashirikisha wadau mbalimbali kwa maslahi ya soka la Iringa na Tanzania kwa ujumla.
Wakati huo huo, TFF imeufungulia Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma ambao sasa utaruhusiwa kutumiwa kwa ajili ya mechi za ligi baada ya kufanya marekebisho kama ilivyotakiwa kikanuni na sheria za soka.
Uwanja huo ulifungiwa kutokana na miundombinu yake kutokidhi matakwa ya kanuni lakini baada ya kukaguliwa imebainika kuwa marekebisho yaliyofanywa yamekidhi vigezo.
TFF imewasisitiza viongozi wa klabu kuhakikisha wanaboresha mazingira ya viwanja vyao vya nyumbani kwa kushirikiana na wamiliki wa viwanja hivyo ili kukidhi vigezo vinavyotakiwa kwa mujibu wa kanuni.
Kimataifa Karia awapongeza viongozi wapya Iringa
Karia awapongeza viongozi wapya Iringa
Read also