Manchester, England
Straika wa Man City, Erling Haaland atakutana na mtaalam baada ya kuumia enka ya mguu wa kushoto juzi Jumapili huku matarajio yakiwa ni kupona na kuitumikia timu hiyo msimu huu.
Haaland aliumia enka Jumapili kwenye mechi ya Kombe la FA dhidi ya Bournemouth, mechi ambayo Man City iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kutinga hatua ya nusu fainali.
Haaland alitolewa uwanjani dakika ya 61 akiwa tayari ameifungia City bao la kusawazisha na baadaye alionekana kwenye vyanzo mbalimbali vya habari akitoka uwanjani huku anachechemea.
Taarifa ya Man City ilieleza kuwa ni matarajio yao kumuona mchezaji huyo akiiwakilisha timu hiyo katika mechi za msimu huu ikiwamo ile ya Kombe la Dunia la Klabu.
Kwa mujibu wa Man City, Haaland ambaye tayari ameifungia timu hiyo mabao 30 katika mechi 40 msimu huu, jana Jumatatu alipelekwa kwa mtaalam kwa lengo la kujua ukubwa wa tatizo alilolipata.
Katika mechi ya Jumapili, Haaland alikosa penalti na nafasi mbili za kufunga kabla ya kufunga bao la kusawazisha na baadaye Omar Marmoush kuongeza la pili lililoifanya City ikate tiketi ya nusu fainali.
Msimu huu si mzuri kwa City na Kombe la FA ndilo taji pekee litakalowanusuru mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England wakiwa tayari wametolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Carabao.
Kimataifa Haaland apelekwa kwa mtaalam
Haaland apelekwa kwa mtaalam
Read also