Cairo, Misri
Simba kesho Jumatano Aprili 2, 2025 inaanza kuisaka tiketi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa ugenini kuumana na Al Masry ya Misri huku kocha wa timu hiyo Fadlu Davids akikiri mechi itakuwa ngumu.
Wawakilishi hao pekee wa Tanzania katika michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) tayari wapo nchini Misri kwa takriban wiki moja sasa.
Simba baada ya mechi hiyo ya kwanza ya hatua ya robo fainali watarudiana na Al Masry Aprili 9 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Davids anaamini uzoefu walioupata kwa kuwa kwao nchini Misri kujiandaa na mechi hiyo utakuwa na manufaa kwao ingawa mechi itakuwa ngumu.
Kocha huyo ambaye alijiunga na Simba Julai mwaka jana amefanikiwa kutengeneza timu iliyotoa ushindani ambayo imemaliza mechi zake za hatua ya makundi ikiwa kinara wa kundi lake.
Akizungumzia matarajio yake katika hatua ya robo fainali, Davids kupitia mahojiano yaliyochapishwa kwenye mtandao wa CAF alisema kila mechi itakuwa ngumu lakini yuko tayari kwa changamoto ya michuano hiyo pamoja na ligi ya ndani.
Baada ya kupangwa kuanza na Al Masry katika robo fainali, Davids alisema walimkubali mpinzani huyo wakitambua kuwa kwa hatua waliyofikia kila timu unayopangiwa ni ngumu.
“Tumemkubali mpinzani wetu, kila timu utakayocheza nayo itakuwa ngumu na wao wanafanya vizuri kwenye ligi ya nchini Misri, mechi itakuwa ngumu hasa unapocheza mbali na nyumbani,” alisema Davids.
Davids licha ya kukiri ugumu huo pia aliendelea kusisitiza kwamba wamefanya maandalizi ya mchezo huo nchini Misri na kujizoesha vyema na mazingira pamoja na kucheza na baadhi ya timu za nchini Misri.
“Mechi haitokuwa rahisi ni kama zilivyo mechi nyingine za robo fainali lakini tuko tayari,” alisema Davids.
Akizungumzia umuhimu wa kuwa kinara katika kundi lake, Davids alisema hilo ni jambo zuri kwani inakupa nafasi ya kucheza mechi ya pili kwenye uwanja wa nyumbani mbele ya mashabiki wako na hivyo kuwa faida.
“Hilo ni jambo zuri unacheza ugenini kwanza na kwa aina ya matokeo unajua nini cha kufanya na kukitarajia na aina ya matokeo unayohitaji ili kufuzu,” alisema.
Davids alifafanua kwa kusema kwamba wanapokuwa mbele ya mashabiki wao Dar es Salaam itawapa faida ya kucheza mechi ya pili nyumbani kwani wanafahamu kuwa katika mashindano haya inapofikia hatua ya robo fainali mechi zinakuwa ngumu hasa unapocheza ugenini.
“Ni lazima uwe katika ubora kwa kila sekunde ya mchezo ili uweze kufuzu hatua inayofuata,” alisema Davids.