Manchester, England
Nahodha wa Man United, Bruno Fernandes amemjibu bilionea na mmiliki mwenza wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe katika madai yake kuhusu baadhi ya wachezaji aliodai wanalipwa fedha nyingi.
Bilionea huyo pia aliwataja wachezaji wengine akidai si wazuri kiasi cha kutosha ingawa wanalipwa fedha nyingi ambapo Fernandes alimjibu kwamba ni klabu ndiyo inayokubali kusaini mikataba na wachezaji hao.
Fernandes ametoa kauli hiyo huku kukiwa na kumbukumbu ya kiungo huyo kupongezwa na bilionea huyo katika mahojiano akimtaja kuwa ni mchezaji mahiri wa soka.
Akifafanua Fernandes ambaye Alhamisi iliyopita alifunga mabao matatu (hat trick) na kuiwezesha Man United kupata ushindi wa jumla wa mabao 5-2 dhidi ya Real Sociedad katika Europa Ligi, pia aliwatetea wachezaji wenzake.
“Ukweli ni kwamba si vizuri kusikia baadhi ya mambo, sidhani kama kuna mchezaji ambaye anapenda kusikia shutuma au mambo yanayozungumzwa kumhusu, eti hauko vizuri kiasi cha kutosha na unalipwa fedha nyingi au mambo mengine kama hayo,” alisema Fernandes.
Fernandes alisema kila mchezaji ana mkataba wake na klabu imekubali kusaini mikataba wakati mchezaji anapokuja au anaposaini mkataba mpya na kwamba hayo ni mambo binafsi yanayomhusu mchezaji mmoja mmoja ambaye anatakiwa kuonesha ubora wake.
Wakati Ractliffe akimsifia Fernandes, nahodha wa zamani wa Man United, Roy Keane amemponda kiungo huyo kutoka Ureno akisema si mpambanaji na hata kipaji alichonacho bado hakitoshi.
Akizungumzia hoja ya Roy Keane, Fernandes alisema kila mtu ana mawazo yake na yeye hawezi kubadili hilo badala yake anachotakiwa kufanya ni kwenda uwanjani na kujaribu kufanya kilicho bora kadri awezavyo kwa ajili ya klabu.