Na mwandishi wetu
Timu ya wasichana chini ya miaka 17 ya Tanzania ‘Serengeti Girls’ imeshindwa kutamba katika kuwania kufuzu Kombe la Dunia baada ya kulala kwa mabao 3-0 mbele ya Zambia.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumapili hii Machi 9, 2025 kwenye Uwanja wa Azam Complex, wenyeji Serengeti walionesha matumaini kipindi cha kwanza na timu hizo kutoka uwanjani zikiwa hazijafungana.
Zambia au Copper Princesses walianza kuinyanyasa Serengeti Girls dakika ya 64 kwa bao la Grace Phiri kabla ya kuongeza la pili dakika ya 80 lililofungwa na Mercy Chipasula.

Matumaini ya Serengeti kupata japo bao la kufutia machozi hayakuwezekana badala yake timu hiyo ilibugizwa bao la tatu lililofungwa na Mercy tena safari hii kwa penalti katika dakika ya 89.
Timu hizo zinatarajia kurudiana Jumamosi ijayo mjini Ndola, Zambia kwenye dimba la Levy Mwanawasa na baada ya hapo mshindi baina ya timu hizo ataumana na mshindi wa mechi kati ya DR Congo na Benin.
Katika mechi nyingine ya kuwania kufuzu fainali hizo, Cameroon ikiwa nyumbani iliilaza Ethiopia mabao 5-2.
Fainali za Kombe la Dunia kwa timu za wasichana chini ya miaka 17 zinatarajia kuchezwa Oktoba mwaka huu nchini Morocco.