Na Hassan Kingu
Mashabiki Simba na Yanga wanacharurana kuelekea mechi yao ya Jumamosi Machi 8, 2025, kila upande ukitamba kuwa bora kumshinda mwenzake lakini namba ambazo haziongopi zina jibu tofauti.
Kwa mujibu wa namba ubora wa timu hizo katika Ligi Kuu NBC msimu huu hautofautiani kwa sana, ukweli wa namba unatupa picha tofauti kuhusu majigambo na kuzodoana kunakoendeea mitaani baina ya mashabiki wa timu hizo.
Mashabiki wangezifanyia tafakuri namba, wangekuwa na hofu kuelekea mechi ya Machi 8 badala ya kujigamba na kuzodoana kwa kuwa ukiziangalia timu zote 16 za kwenye ligi, Yanga na Simba ndizo zenye muendelezo mzuri wa ushindi.
Yanga inashika usukani wa ligi hiyo ikiwa na pointi 58 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 54, hivyo tofauti baina ya timu hizo ni pointi nne.
Pointi nne ni nyingi lakini Simba ipo nyuma kwa mchezo mmoja, imecheza mechi 21, Yanga imecheza mechi 22, kutokana na ubora wa timu hizo kwa namna zinazovyoshinda mechi zao tofauti yao kimsingi ni pointi moja.
Tunaamini Simba watashinda kama wanavyoshinda Yanga dhidi ya timu nyingine, hivyo tofauti itabaki pointi moja ambayo kimsingi ni ndogo na rahisi kuipoteza wakati wowote.
Maana yake ni kwamba mashabiki Yanga hawana sababu ya kujiamini kwamba wameshalibeba taji la ligi kwa mtaji wa pointi moja ambayo wanaweza kuipoteza wakati wowote, ni hivyo hivyo kwa Simba wapo nyuma kwa pointi moja na wana kazi ya kuisaka.
Kwa kuziangalia namba maana yake ni kwamba mechi ya Machi 8 inabaki kuwa muhimu kwa timu zote kuhakikisha zinashinda, ikishinda Yanga itakuwa faida zaidi kwani tofauti itakuwa ya pointi nne zenye uhakika si sawa na hizi za sasa wakati Simba ina kiporo cha mechi moja.

Ni hivyo hivyo ikishinda Simba itakuwa imeisogelea Yanga na kujitofautisha kwa pointi moja ya uhakika na kama wote wataendelea kushinda mechi zao hadi ligi itakapofikia tamati maana yake ni kwamba Simba italibeba taji ikiitangulia Yanga kwa pointi mbili.
Kwa shabiki ambaye ataziangalia timu hizo kwa kuzichambua namba atauona ukweli wa pointi hizo ulivyo na ambavyo utazitesa timu hizo, tofauti kwa sasa ni pointi moja au mbili.
Matokeo ya sare baina ya timu hizo kidogo yatakuwa msaada kwa Yanga kwa kuwa itajinasua katika tofauti ya pointi moja na kutanguliwa mechi moja badala yake itakuwa pointi moja ya uhakika ambayo hata hivyo ugumu wake upo pale pale. Ukipoteza mechi moja tu umwekwisha, ukitoka sare moja tu umejiweka pabaya.
Vyovyote itakavyokuwa Yanga inatakiwa kushinda mechi ya leo ili kujiweka pazuri katika kulibeba taji kama ambavyo Simba inatakiwa kushinda ili kuwaweka Yanga pagumu katika mbio za kulibeba taji.
Nje ya namba za pointi kuna namba za magoli, hapa ndipo Yanga wanapoweza kujivunia kwani wamewaacha Simba kwa tofauti ya mabao 12, Yanga wana mabao 48, Simba 36, hii inaweza kuwa faida kubwa kama timu zitafungana pointi.
Yanga hata hivyo hawawezi kuangalia idadi ya mabao hayo ni kujiaminisha kuwa ni mtaji wa kulibeba taji badala yake wanatakiwa kuendelea na wimbi la ushindi katika mechi zao zilizobaki, hapo tu wataweza kulitetea vyema taji hilo.
Namba nyingine
Namba nyingine ni za mabao ya kufungwa, Simba ina ahueni kwani imefungwa mabao manane dhidi ya Yanga iliyofungwa mabao tisa, lakini pia hii haiwezi kuwa na maana yoyote badala yake kila timu inatakiwa kushinda mechi zilizo mbele yake.
Pia kuna namba za uwiano wa mabao, Yanga ikiwa 49 Simba 38, hizi namba mwisho wa siku pia haziwezi kuwa na maana yoyote badala yake la muhimu ni timu kupata ushindi.
Ukiachana na namba za pointi ambazo ni muhimu kuliko namba zozote kwenye ligi, namba nyingine yaani za mabao ya kufunga, kufungwa na uwiano zitakuwa na maana tu pale timu zitakapofungana pointi katika mechi zao za mwisho.
Ili kujitoa katika namba hizo ngumu na zinazoleta hofu za kulibeba taji, tunajikuta tukirudi katika hoja ile ile ya kwamba kila timu inatakiwa ishinde kila mechi, na mtaji wa kwanza muhimu kuushinda ni hii mechi yao ya Machi 8.