Na Hassan Kingu
Utata umeibuka kuhusu mechi ya Simba na Yanga ambayo imepangwa kuchezwa leo Jumamosi Machi 8, 2025 na huenda mechi hiyo isichezwe baada ya Simba kuzuiwa kufanya mazoezi.
Yanga ambao ni wenyeji wa mechi hiyo wanadaiwa kuwazuia Simba kufanya mazoezi siku moja kabla ya mechi kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi ingawa nao wametoa taarifa leo Jumamosi wakisisitiza mechi ipo kama kawaida.
Simba katika raarifa yao walielezea kitendo cha kuzuiwa kufanya mazoezi na kuitaja kanuni ya ligi kuu inayotaka timu mgeni kufanya mazoezi kwenye uwanja itakayochezwa mechi angalau siku moja kabla ya mechi.
Katika hoja yao Simba wanadai kunyimwa fursa ya kufanya mazoezi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na wenyeji wa mechi Yanga kwa makusudi licha ya kufika uwanjani katika muda husika.
Baada ya kufika uwanjani Ijumaa kwa ajili ya mazoezi, waliarifiwa na meneja uwanja kuwa hana maelekezo ya kuruhusu mazoezi kufanyika bila ya taarifa ya kamishna wa mchezo husika.

Katika hali ambayo haikutarajiwa, Simba katika taarifa yao wanadai kuwa hata baada ya kamishna wa mchezo kufika, mabaunsa wanaoaminika kuwa wa Yanga walizuia msafara wa Simba kuingia uwanjani hapo kufanya mazoezi.
Iliwachukua Simba saa takriban mbili kutafuta ufumbuzi wa suala hilo lakini jitihada zao hazikuzaa matunda na hatimaye wakaamua kuondoka eneo hilo kwa sababu walizozitaja kuwa ni za kiusalama.
Kutokana na sakata hilo, Simba wameahidi kutoshiriki katika mchezo wao na Yanga na kutaka hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wahusika wote.
Taarifa ya Yanga
Baada ya uamuzi huo wa Simba, Yanga nao wametoa taarifa wakisisitiza kwamba mchezo wao dhidi ya Simba uliopangwa kufanyika leo Jumamosi ya Machi 8, 2025 upo pale pale kama ilivyopangwa na hakuna mabadiliko yoyote.
Yanga kama wenyeji wa mchezo wamedai kufuata taratibu zote husika kama inavyoelekezwa kwenye kanuni za ligi hiyo na maandalizi yote yapo tayari.

Zaidi ya hilo uongozi wa Yanga umeahidi kupeleka timu uwanjani na hautakuwa tayari kucheza mchezo huo siku nyingine tofauti na leo yaani Jumamosi ya Machi 8, 2025.
Wakati Yanga wakitoa kauli hiyo, kiongozi mmoja mwandamizi wa Simba amenukuliwa katika vyanzo mbalimbali vya habari akisema kwamba Simba hawatopeleka timu hadi wahusika wa kadhia hiyo watakapoadhibiwa na mamlaka husika za soka.
Mazingira yote hayo yanaifanya mechi hiyo maarufu kwa jina la Kariakoo au Dar Derby kuwa njia panda hadi wakati huu.