Manchester, England
Kocha wa Man United, Ruben Amorim amesema uongozi wa klabu hiyo hautompa muda wa kutosha kuifanyia maboresho timu kama ambavyo klabu ya Arsenal imempa kocha wao, Mikel Arteta.
Arteta alikabidhiwa rasmi majukumu ya kuinoa Arsenal Desemba 2019 akichukua nafasi ya Unai Emery na kuanzia kipindi hicho hadi sasa ameweza kuifanya timu hiyo kuwa miongoni mwa timu tishio katika mbio za kusaka mataji.
Kwa upande wake Amorim ambaye huu ni msimu wake wa kwanza Man United, haamini kama na yeye atapata muda kama wa Arteta ambaye matunda ya kazi yake yameanza kuonekana.
Tangu akabidhiwe jukumu la kuinoa Arsenal, Arteta ameiwezesha timu hiyo kubeba taji la FA mwaka 2020 lakini ameendelea kuhaha kulisaka taji la Ligi Kuu England na ingawa hajafanikiwa, ubora wa kikosi chake unaonekana.
Arteta pia tangu ajiunge na Arsenal timu ambayo aliwahi kuichezea miaka ya nyuma, imemchukua misimu mitatu kuirudisha timu hiyo katika fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
“Sitoweza kupewa muda kama ambao Arteta amekuwa nao, naiona Arsenal ni klabu tofauti kwa mapana na namna kwa ambavyo Arteta anakabiliana na mambo inatia hamasa kwa kila mtu,” alisema Amorim.
Arsenal, kesho Jumapili itakuwa ugenini Old Trafford kuikabili Man United, timu ambayo inakabiliwa na janga la wachezaji wao tegemeo kuwa majeruhi, wachezaji hao ni Mason Mount, Luke Shaw na Lisandro Martinez.
Kwa upande mwingine Arsenal imeonekana kuwa moto kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Jumanne iliyopita iliinyuka PSV Eindhoven mabao 7-1 wakati siku mbili baadaye, Man United iliambulia sare ya bao 1-1 mbele ya Real Sociedad katika Europa Ligi.