Na mwandishi wetu
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ameipongeza kamati mpya ya utendaji Chama cha Soka Mara (FAM) iliyochaguliwa kwenye kwenye mkutano mkuu wa uchaguzi uliofanyika hivi karibuni mkoani Mara.
Viongozi wapya waliochaguliwa ni Mussa Nyamandege ambaye ameshinda nafasi ya mwenyekiti na Harub Salum ambaye ameshinda nafasi ya makamu mwenyekiti.
Wengine waliochaguliwa kupitia uchaguzi huo na nafasi zao kwenye mabano ni Augustine Mgendi (mjumbe mkutano mkuu TFF) na Hollo CHarles na Paschal Chiganga (wajumbe wa kamati ya utendaji).
Karia ameahidi kuwapa ushirikiano viongozi hao wapya wa FAM na kuwataka wasimamie maendeleo ya mpira wa miguu mkoani Mara.
Wakati huo huo TFF wameufungia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora baada ya kubainika kuwa haukikidhi vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.
Taarifa ya TFF iliyopatikana Ijumaa hii ilieleza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kubaini kuwa uwanja huo haukidhi matakwa kama ilivyoanishwa kwenye masharti ya kanuni ya leseni za klabu.
Kutokana na uamuzi huo, timu zote zinazotumia uwanja huo kwa mechi zao za ligi kama uwanja wa nyumbani zitalazimika kutafuta uwanja mwingine kama kanuni zinavyoelekeza.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na ofisa habari na mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo, uamuzi huo utabaki hivyo hadi uwanja huo utakapofunguliwa baada ya kufanyiwa marekebisho na kukaguliwa na TFF.
TFF kupitia taarifa hiyo pia imeendelea kuzikumbusha klabu umuhimu wa kutunza na kuboresha miundombinu ya viwanja.
Soka Karia awapongeza mabosi wa soka Mara
Karia awapongeza mabosi wa soka Mara
Read also