Madrid, Hispania
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amekiri timu yake imepata pigo kubwa katika mbio za kusaka taji la La Liga baada ya kufungwa mabao 2-1 na Real Betis jana Jumamosi.
Katika mechi hiyo, Real Madrid ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na
Brahim Díaz lakini Betis walisawazisha kupitia kwa Johnny Cardoso na kuzifanya timu ziende mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Kipindi cha pili, nyota wa zamani wa Real Madrid, Isco aliifungia Betis bao la pili kwa penalti na kuifanya Real Madrid ipoteze pointi tatu na kujiweka pagumu katika mbio za kulisaka taji hilo dhidi ya timu za Barcelona na Atlético Madrid.
Akizungumzia matokeo hayo, Ancelotti alisema mechi ilikuwa mbaya kwao licha ya kuanza vizuri lakini hawakuweza kuendelea na kasi yao hivyo kushindwa na timu ambayo ilicheza vizuri na ilikuwa haki yao kushinda.
“Hili ni pigo kubwa, lazima tuchukue hatua, kupoteza mechi katika hatua hii ya msimu ni pigo, hatukufanya vizuri, tulipoteza mpira mara 27 katika kipindi cha kwanza, hicho ni kiasi kikubwa,” alisema Ancelotti.
Ancelloti pengine baada ya kuona mambo yanakuwa magumu dakika ya 75 alimtoa Kylian Mbappe na kumuingiza Endrick, mabadiliko ambayo hayakuweza kubadili matokeo ya mchezo huo.
Kocha huyo hata hivyo baadaye alisema kwamba Mbappe alikuwa na tatizo la jino na hata mazoezi hakufanya vizuri na alimtoa na kumuingiza Endrick ili kuepusha matatizo zaidi.
Real Madrid kwa sasa inapigania mataji matatu, Jumatano iliyopita ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Real Sociedad katika nusu fainali ya Copa del Rey na keshokutwa Jumanne itacheza mechi ya hatua ya 16 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid.