Manchester, England
Kocha wa Man United, Ruben Amorim amewaambia wazi wachezaji wake kuwa wengi wao watalazimika kuachwa mwishoni mwa msimu katika mpango wa kuipangua na kuisuka upya timu hiyo.
Mazingira magumu ya kifedha ya klabu hiyo kwa kipindi hiki yanamaanisha kwamba ili waweze kusajili wachezaji wapya lazima wapate pesa baada ya kuuza wachezaji walionao sasa.
Katika hilo, Amorim ameweka wazi kuwa atalazimika kuwa mkweli kwa wachezaji wake kama anaona wanafaa kuendelea kuwa nao katika klabu hiyo ya Old Trafford.
Amorim hata hivyo alisema kwamba kwa sasa hawawezi kuzungumzia suala la wachezaji kuachwa kwa kuwa bado wana mechi nyingi za kucheza lakini jambo hilo lipo wazi.
Kocha huyo pia alifafanua kwamba anadhani jambo hilo ni muhimu kwa sababu kila mmoja anafahamu katika soka kuna wakati unabaki na kuna wakati unalazimika kuondoka.
“Unapokuwa mkweli kwa mwenzako hapo anaweza kukubaliana na hali, mwanzoni ni vigumu lakini wataelewa, kwa hiyo nipo wazi na mkweli kwa wachezaji wangu na tayari wanafahamu kwamba kuna watalaolazimika kuondoka mwishoni mwa msimu,” alisema Amorim.
Ukosefu wa fedha unadaiwa kumfanya Amorim, kocha mwenye umri wa miaka 40 aione kazi yake kuwa ngumu na sasa amejikuta njia panda kutokana na ukubwa wa majukumu aliyonayo.
Amorim ambaye alijiunga na Man United Novemba mwaka jana akitokea Sporting CP ya Ureno hata hivyo alisema kwamba alitambua ukubwa wa majukumu yanayomkabili na ugumu alionao katika kuweka mambo sawa.